Kofia Nyekundu ya 'People Power' ya Bobi Wine, marufuku Uganda

Bobi Wine
Bobi Wine
Jeshi la Uganda limepiga marufuku raia kuvalia kofia nyekundu ambayo hutumiwa kama ishara ya "People Power" na mwanaharakati Bobi Wine.

Vazi hilo la kichwa, ambalo linahusishwa na vugu vugu la Wine, limetajwa kuwa ni mavazi ya jeshi.

Nyota huyo wa zamani wa muziki wa Pop, anatarajia kumrithi Rais Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, alilaani marufuku hiyo.

"Mavazi rasmi yanayojumuisha kofia nyekundi ya Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi wa Uganda (UPDF), umetangazwa kwenye gazeti la kiserikali.

Agizo hilo liliidhinishwa na vyombo vya juu vya kijeshi Uganda ambavyo pia vilipongeza kamati ya mavazi kwa kumaliza kazi iliyopewa miaka ya nyuma," msemaji wa jeshi Richard Karemire alisema .

Aliendelea kusema, "Inaonesha dhamira ya kufafanua kitambulisho na mtazamo wa utalaamu wa kijeshi na kufuata kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki."

Hatua hiyo imekosolewa na Wine ambaye anasema kwamba "Kupigwa marufuku kwa kofia yetu ni hujuma.

"Ni jaribio la wazi la kutishia uhuru tulio nayo," Mwanaharakati huyu mwenye umri wa miaka 37, alisema.

Hata hivyo, Wine alisisitiza kwamba agizo hilo halitakuwa na athari yoyote kwao.

''People Power ina nguvu zaidi ya kofia hiyo nyekundu, sisi wenyewe tuna nguvu kuliko alama yetu. Sisi ni wanaharakati wa kisiasa tunaoibuka kwa kupigania mustakabali wa Uganda na tutaendeleza mapambano yetu ya demokrasia," alisema.

Kofia hiyo,ambayo pia imevaliwa na baadhi ya wanajeshi wa Uganda, iliangaziwa kwenye gazetini rasmi ya taifa kama vazi la jeshi la Uganda.

Agizo hilo pia linanukuu kwa vazi hilo ni "mali ya serikali" ambayo raia hawaruhusiwi kulivalia.

Nchini Uganda, kofia hiyo huvaliwa na raia wanaounga mkono Bobi Wine.

Bob ambaye ameifanya kofia hiyo nyekundu kuwa ishara ya vugu vugu lake, anaeleza ni kama "ishara ya kupinga uongozi mbovu."

Wine amepata uungwaji mkubwa, haswa miongoni mwa vijana wa Uganda ambao wamevutiwa na ukosoaji wake wa Museveni - ujumbe ambao mara kwa mara ameingiza katika nyimbo zake.