‘Kosa kazi ujue wanaokujali’ Aliyopitia Calvin Muga yamemfungua macho ( Part 1 )

Kuna msemo kwamba Nairobi ni shamba la mawe. Hakuna anayeujua msemo huu zaidi ya Calvin Muga  ambaye masaibu  yake yalimfanya kujua usaliti na unafiki wa marafiki  na jamaa zake.

Maisha yalikuwa sawa na ubabe wake ulimpa matumaini kwamba atayapanga maisha yake vizuri baada ya kupata kazi katika shirika moja lisilo la kiserikali mwaka wa 2010 na kisha kuifanya kazi hiyo kwa miaka minnne unusu hadi ghafla kazi hiyo ilipokatika mwaka wa 2014 . Kwa sababu ya kukosa kipato alilazimika kuihama nyumba yake ya chumba kimoja hadi katika nyumba ya bati  aliyotakiwa kulipa shilingi 3000 kwa mwezi kama kodi.

Hapo ndipo safari yake  ya mateso ilipoanza kwa sababu alibisha katika milango ya wote aliowajua ili wampe hifadhi angalau ya mwezi mmoja kabla ya kupata shughuli nyingine lakini hakuna aliyekuwa na muda naye. Kinachompa  machungu hadi sasa ni jinsi watu aliodhania kwamba ni jamaa zake waliofaa kusimama naye wakati wa shida walivyomgeuka .

"Kitu ambacho sitasahau ni majibu niliyopata kutoka kwa watu  niliofikiri walikuwa karibu nami. Sikutaraji majibu yao yangekuwa makali hivyo. Nilichotaka ni hifadhi ya mwezi mmoja tu" anasema  Muga

 Baada ya kutafuta kazi za vibarua bila kukosa, Muga aliamua kwenda mashambani mwaka wa 2015  ili  apate muda wa kutafakari jinsi ya kujikwamua tena atakaporudi jijini. Alimtaka tena rafikiye mmoja wa karibu  ampe hifadhi ya mwezi mmoja tu lakini alimjibu kwamba hangerudi jijini iwapo alifahamu kwamba hana kazi. Hilo lilimkwaza sana Muga lakini imani yake kwa mola na matumaini yake kuhusu mustakabali wake yalimfanya kutokata tamaa.

Muga hakuamini kwamba kukosa kazi Nairobi kunaweza kukufanya ukawa kama mzigo kwa jamaa na rafiki zako . Ameeleza jinsi baadhi ya watu waliokuwa karibu naye walianza kumkwepa pindi walipomuona .  Muga alipatwa na mawazo kupindukia na wakati mwingi angejifungia katika chumba chake  na kulia kwa machungu sana akikumbuka usaliti na mahanaiko aliyopitia.

"Wakati unapokuwa na kila unachotaka, mtacheka sana na wengi na wakati wote utawaona katika maisha yako, kosa kazi  au pesa kisha utake msaada wao, hapo ndipo utakapojua uko pekee yako"alisema Calvin .

Anasema si vibaya kuwa na  marafiki wa karibu au hata  kuzoeana na jamaa zako, lakini ni muhimu ufahamu nia yao ya kujipendekeza kwako kwani usije ukapatwa na mshutuko wakati unapowahitaji  na ukaachwa pekee  yako. Muga alipambana kuanza upya maisha yake aliporejea jijini na baadaye akaanza kufanya kazi yake ya kutoa ushauri kuhusu masuala ya uongozi ya demokrasia. Muda sio mfupi alianza kuona mwanga katika bomba lililokuwa na giza.

Anashangaa kwamba kwa sababu mambo yanamwendea vizuri sasa, jamaa zake na rafiki waliomkwepa wakati hakuwa  na kazi au  pesa, wameanza tena kumkaribia. Anasema hana kinyongo nao kwani amewasamehe lakini sasa ana busara ya kujua jinsi ya kutangamana nao bila kukubalia waingie tena katika maisha yake bila kuwa na manufaa wanayompa. Katika ehemu ya pili ya masimulizi yake, soma kuhusu alivyokutana na mkewe aliyempenda wakati hakuwa na  chochote.‘