Kunani? Malkia Strikers bado hawajapokea marupurupu yao

Timu ya voliboli ya kinadada Malkia Strikers bado hawajapokea marupurupu yao ya michuano ya kombe la dunia ya FIVB nchini Japan, licha ya serikali kuahidi kulipa timu katika kipindi cha masaa 48 kabla ya kuondoka kwa michuano yoyote.

Marupurupu ya Malkia strikers ya michuano ya All Africa Games huko Morocco pia yalichelewa huku baadhi yao wakiyapokea wiki iliyopita. Timu hio pia haijapata malipo yao ya michuano ya kufuzu kwa Olimpiki ya mabara iliyofanyika Italia mwezi Julai.

Hayo yakijiri, afisa mkuu wa Gor Mahia Lordvick Aduda amesisitiza kwamba ni FKF inayopaswa kumtibu mlinzi Philemon Otieno. K'Ogalo na FKF wamekuwa wakivutana kuhusu ni nani anapaswa kulipia gharama ya matibabu ya kiungo huyo ambaye alipata jeraha kabla ya Kenya kuchuana na Tanzania katika mechi ya kufuzu kwa AFCON mwezi Agosti.

Aduda pia anasema FKF haijajibu barua yake kuhusu kucheleweshwa kwa matibabu ya mchezaji huyo.

Kwingineko, nahodha wa timu ya Kenya itakayoshiriki mashindano ya ubingwa wa dunia wa riadha jijini Doha, Qatar, Julius Yego na naibu kocha Bernard Ouma wamesema timu hiyo iko tayari kupambana na wapinzani wao.

Wakati huo huo mipango ya usafiri ya timu hiyo ilibadilishwa katika dakika za mwisho jumatatu na kupelekea serikali kuonya kwamba tikiti ambazo zimetolewa hazitaweza kufutiliwa mbali katika siku zijazo.

Timu hiyo sasa itaondoka kwa awamu, huku ya kwanza inayojumuisha wanariadha 19 ikitarajiwa kuondoka nchini hii leo.

Soma uhondo zaidi: