bangi

Kung’uta miwa! Uganda yaidhinishwa kusafirisha bangi ulaya

Wakaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) wameidhinisha Uganda kutuma bidhaa za bangi barani Ulaya, gazeti la Daily Monitor linaripoti.

Bangi itakayotumwa kwenye soko la Ulaya hata hivyo si kwa matumizi ya starehe kama uvutaji bali ni kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa Monitor mainspekta wa bidhaa za matibabu zitokanazo na bangi kutoka Uholanzi walikagua mashamba ya bangi kwenye wilaya za Hima na Kasese kati aya Julai 29 na Agosti 4.

Maafisa hao kabla ya kuondoka Uganda waliikabidhi cheti cha kukidhi vigezo kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd kwa kipindi cha Agosti 6, 2019 mpaka Agosti 5, 2020.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Benjamin Cadet amelithibitishia gazeti hilo kuwa EU wamewapa idhini ya kuasafirisha bangi Ulaya.

“Baada ya EU kuthibitisha bidhaa zetu – usafirishwaji na mnyororo wote wa uzalishaji – kuanzia kupanda mpaka kuvuna kwa bangi utafanyika kikamilifu nchini Uganda na kupelekwa kwenye masoko ya Ulaya,” Cadet amesema.

Takribani kampuni 50 zimeomba kibali Wizara ya Afya kuungana na kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd ili kuzalisha bangi kwa ajili ya matibabu.

Bangi inayozalishwa Uganda katika shamba la wilayani Kasese ina virutubisho vya Cannabinol (CBD) na Tetrahydrocannabinol (THC) ujazo wa 2.7mg THC na 2.5mg CBD mtawalia. Virutubisho hivyo vimepasishwa Ulaya, Marekani na Canada.

Wavutaji bangi
Image captionUzalishaji na matumizi ya bangi kwa starehe (uvutaji) bado yamepigwa marufuku Uganda

Uganda ilishindwa kusafirisha bangi ya thamani ya dola 600 milioni kwenda Canada na Ujerumani mwezi Julai mwaka huu baada ya kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd kutokuwa na cheti kutoka EU.

Uganda ndio nchi pekee Afrika Mashariki ambayo imehalalisha uzalishaji wa bangi, japo kwa matumizi ya kiafya.

Mwezi Mei mwaka huu, Mbunge wa Kahama mjini nchini Tanzania, Jumanne Kishimba aliitaka serikali kuhalalisha matumizi ya bangi nchini Tanzania kwa mautumizi ya dawa.

”Tunavyozungumza, Uganda imehalalaisha upanzi wa Marijuana kwa matumizi ya dawa”, alisema akitaja ripoti za hivi majuzi kwamba taifa hilo la Afrika mashariki limenunua mbegu kupanda mmea huo.

”Sijui ni kwa nini kitengo cha chakula na dawa hakijachukua sampuli kuelezea serikali kwamba dawa hizo zina bangi ndani yake”, alihoji.

Hata hivyo serikali ya Tanzania imepinga uwezekano wowote wa kuhalalishwa kwa mmea huo katika taifa hilo.

-BBC

Photo Credits: BBC

Read More:

Comments

comments