Kwa nini ripoti ya BBI imecheleweshwa kukabidhiwa Uhuru na Raila?

Uhuru na Raila
Uhuru na Raila
Shajara ya rais Uhuru Kenyatta juma hili inaonesha kwamba shughuli chungu nzima imeratibiwa na nafasi ya kukabidhiwa ripoti ya BBI ni finyu.

Kumekuwa na wingu la matarajio kwamba rais pamoja na kinara wa ODM Raila Odinga wangekabidhiwa ripoti ya BBI juma hili baada ya kukamilika kwa uchaguzi mdogo wa Kibra Ijumaa iliyopita.

Tume ya maridhiano na uwiano ilikamilisha kuandika mapendekezo majuma matatu yaliyopita, huku wakisema kwamba 'ripoti itakabdihiwa nafasi itakapopatikana.'

"Tayari tumewasiliana na afisi ya rais kwamba mapendekezo ya BBI yako tayati kukabidhiwa rais," ujumbe uliotiwa saini na Paul Mwangi na mwenzake Martin Kimani ulisoma.

Kucheleweshwa kwa ripoti hiyo kukabidhiwa viongozi hao wawili kumewadia kipindi ambacho kuna tetezi kwamba baadhi ya mapendekezo kwenye ripoti hiyo 'yanafaa kufutiliwa mbali.'

Kulingana na taarifa kutoka baadhi ya waliochangia ripoti hiyo, inasema kwamba baadhi ya mapendekezo yanatathminiwa kwa kuwa yataleta mgawanyiko zaidi kwenye serikali.

Tayari viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya wameonya kupinga mapendekezo hayo iwapo yatapendekeza rais kuchaguliwa bungeni kinyume na ilivyo sasa ambapo rais huchaguliwa na wakenya kwa njia ya kura.

Kulingana na hali ilivyo sasa, rais anamsururu wa makongamano na warsha kadhaa ikiwemo kukutana na wajumbe waliohudhuria kongamano la ICPD25 linaloendelea.

Alhamisi asubuhi, rais Uhuru anatarajiwa kukutana na waziri wa masuala ya kigeni wa Jamhuri ya Czech Thomes Petrricek.

Mnamo Ijumaa, rais anatarajiwa katika uzinduzi wa mkutano wa kanda kuhusu ajira kwa vijana.