Lengo la Man City ni kufuzu katika ligi ya mabingwa - Guardiola

Pep Guardiola anasema lengo la Manchester City ni kujikatia tikiti katika ligi ya mabingwa msimu ujao baada ya matumaini yao ya kushinda taji msimu huu, kudidimizwa hata zaidi na Crystal Palace.

Bao la kujifunga la Fernadinho kunako dakika ya 90 lilihakikishia Eagles sare uwanjani Etihad. Matokeo hayo yanawaacha City alama 13 nyuma ya viongozi wa ligi ya Primia Liverpool ambao wana mechi mbili mkononi na watachuana na Manchester United leo. 

Katika mechi zingine, Gunners walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Sheffield United na kusalia nambari kumi katika jedwali. Chelsea nao walinyukwa bao moja na Newcastle katika uga wa St. James Park.

Real Madrid walipanda alama tatu juu ya mabingwa Barcelona kileleni mwa La Liga baada ya ushindi wao dhidi ya Sevilla ugani Bernabeu. Kiungo wa kati wa Brazil Casemiro alifunga mabao mawili na kukisaidia kikosi hicho cha Zinedine Zidane. Barcelona hata hivyo wana fursa ya kurege kileleni kwa tofauti ya mabao watapowaalika Granada leo.

Beki wa kushoto wa Paris St-Germain Layvin Kurzawa mwenye umri wa miaka 27, ametoa ishara kwamba anakaribia kujiunga na Arsenal mwezi huu baada ya kutangaza kwamba amejiunga na ajenti mmoja wa Uingereza. Wakati huo huo Arsenal wamekubali mkataba wa miaka mitano na Kurzawa, huku beki huyo akitarajiwa kuondoka PSG mwisho wa msimu.

Kenya Morans jana waliwacharaza mahasimu wao Sudan Kusini 74-68 katika mechi ya kusisimu ya michuano ya FIBA Afro uwanjani Nyayo. Mechi hio iliahirishwa kwa lisaa limoja baada ya mashabiki kufurika katika ukumbi huo kutizama mechi hio. Kenya sasa imefuzu kwa awamu inayofuata ya michuano hiyo ya kufuzu, baada ya kumaliza bila kushindwa.

Naivas FC itapambana na mabingwa wa KPL Gor Mahia katika kombe la betways FKF, baada ya kuilaza chipukizi wa Kariobangi Sharks 3-0 jana katika awamu ya mchujo.  Mabingwa watetezi Bandari nao watailika KSG Ogopa  ambao waliwanyuka FC Re-union 2-0. Mechi 14 za mchujo zitachezwa leo huku  Nairobi Water ikikwaruzana na Zetech Titans, Jericho Revelation wakipambana na timu ya wanaharabri Nation FC, huku Kenpoly ikinyanyuana na Mwatate United. Washindi watafuzu kwa awamu ya  mchujo ya 32 bora.

Conor McGregor alirejea katika ukumbi wa  Octagon kwa kishindo baada ya kumbwaga Donald "Cowboy" Cerrone wa Merikani kwa sekunde 40  katika pigano lao la UFC liloangaziwa zaidi jijini Las Vegas.  Mzaliwa huyo wa Ireland  alimshinda mpinzani wake bila kuanguka sana licha ya Donald kuwahakikishia mashabiki kuwa angembwaga Conor.