LIGI KUU UINGEREZA: Waniaji wa taji ya mchezaji na meneja bora wa mwezi wajulikana

Ligi kuu ya uingereza imetangaza majina ya wachezaji na mameneja watakao wania taji ya mchezaji na meneja bora wa mwezi wa Agosti. Si jambo la kushangaza kuwa waniaji wanatoka timu ambazo zinatia fora katika ligi kuu msimu huu. Mashindano yanakisiwa kuwa mkali kati ya wakilishi wa Chelsea na Swansea kwani timu hizo zimeweza kushinda mechi zao zote za ligi kuu kufikia sasa huku Chelsea wakiongoza jedwali kwa sababu ya utofauti wa mabao.

Miongoni mwa waniaji ya taji ya mchezaji bora wa mwezi, timu za Chelsea na Swansea zimewakilishwa na wachezaji wawili kila moja kufuatia kuorodheshwa kwa Diego Costa, Cesc Fabregas, Gylfi Sigurdsson na Nathan Dyer.

Andreas Weimann wa Aston Villa alikamilisha orodha hiyo na ikiwa ataibuka mshindi atakuwa mchezaji wa kwanza wa Aston Villa kubeba taji hiyo tangu Ashley Young apewe tuzo hiyo Septemba 2008. Cesc Fabregas (Januari 2007 na Septemba 2007) na Gylfi Sigurdsson (Machi 2012) wamewahi kubeba taji mbeleni huku Diego Costa na Nathan Dyer wakitarajia kuishinda kwa mara ya kwanza.

Taji la meneja bora wa mwezi ina waniaji nne; Jose Mourinho (Chelsea), Garry Monk (Swansea), Paul Lambert (Aston Villa) na Mark Hughes (Stoke City). Jose Mourinho anatarajia kushinda taji hiyo kwa mara ya nne na kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2007. Kama Mourinho, Mark Hughes pia alishinda taji hiyo mara ya mwisho mwaka wa 2007 na ikiwa atafaulu wakati huu ataingia katika vitabu vya historia kama meneja wa kwanza wa Stoke City kupewa heshima hiyo. Garry Monk na Paul Lambert hawajawahi shinda taji hiyo mbeleni.