Ligi ya mabingwa ulaya kung'oa nanga leo usiku

Leo ni leo manake msema kesho ni mwongo. Mashabiki wa ligi ya mabingwa ulaya huenda wakakosa usingizi usiku wa leo kwani mwendo wa saa nne usiku ligi hiyo ya msimu wa 2019/2020 unatarajiwa kuanza leo, huku klabu ambazo kwa miongo kadhaa sasa imeonekana kubobea katika ligi hiyo, watakuwa wanapimana nguvu usiku wa leo.

NAPOLI VS LIVERPOOL

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo vijana wake Jurgen Klopp watakuwa wanazamia uwanjani San Paolo nyumbani kwake Napoli. Usisahau kabla Liverpool kuibuka mshindi msimu uliopita, waliweza kufika fainali msimu wa 2017/2018 ambapo Real Madrid waliwashinda na kujinyakulia kombe hilo. Napoli pia chini ya mkufunzi wao Carlo Ancelloti wanatarajiwa kuleta ushindani mkubwa. Je, Liverpool watawabwaga Napoli?  Upande wangu naona wakitoka sare tasa.

BORUSSIA DORTMUND VS BARCELONA

Vijana wake Lucien Favre watakuwa wanawakaribishwa wanacatalonia nyumbani kwao Signal Iduna Park, mechi ambayo itakuwa inatazamwa na mashabiki wengi kwani msimu uliopita, Barcelona walitolewa na Liverpool katika nusu fainali ya kombe hilo huku ikiwa ni miaka nne sasa baada ya Barcelona kubeba taji hilo. Barca ambao walimsajili mshambulizi Antoine Griezmann, inatarajiwa kuonyesha makali yake usiku huu. Utabiri wangu Barca watawapiga Dortmund mabao tatu kwa moja.

ATLETICO MADRID VS JUVENTUS

Ni mechi ambayo klabu ambazo zinatawala katika ligi tofauti watakuwa wanapatana. Isije ikasahaulika kuwa klabu hizi zote hazikufika semi fainali ya msimu uliopita, je msimu huu wamejiandaa kiasi cha kiwango gani? Yote hayo leo usiku uwanjani Wanda Metropolitano nyumbani kwake Atletico, huku klabu ya Juventus wakiwa na matarajio makubwa kuwa msajili wao kutoka Real Madrid Cristiano Ronaldo atachangia pakubwa wao kushinda mchuano huo. Utabiri wangu ni wana Atletico watawashinda Juventus kwa mabao mawili kwa moja.

PARIS SAINT GERMAIN VS REAL MADRID

Ni mechi kali zaidi usiku wa leo ambapo klabu hizi mbili zitapimana makali uwanjani Le Parc des Princes nyumbani kwake PSG. Neymar, Mbappe, na Cavani ambao ni washambulizi wa PSG, wanatarajiwa kufunga mabao ili kuipa klabu hiyo ushindi usiku wa leo. Zinedine Zidane ambaye ni mkufunzi wa klabu ya Real Madrid atakuwa anatarajiwa kumchezesha msajili wake kutoka klabu ya Chelsea Eden Hazard, huku akisaidiana na Karim Benzema, na Vinicious Junior. Katika mchuano huo, utabiri wangu ni vijana wa PSG watashinda mechi hiyo kwa mabao tatu kwa mawili.