Liverpool

Ligi ya Primia (EPL) inatarajiwa kurejea Juni 17

Ligi kuu ya soka nchini Uingereza inatarajiwa kurejea Juni 17 mwaka huu.

Pazia la ligi hiyo litafunguliwa kwa mechi mbili, mtanange baina ya Manchester City dhidi ya Arsenal na Aston Villa dhidi ya Sheffield United.

Mechi hizo mbili ni za viporo.

Ratiba kamili itaanza wikiendi ya Juni 19-21.

Klabu zinazoshiriki ligi hiyo bado zinaendelea na mjadala wa namna ya kurejea kwa ligi katika mkutano unaoendelea hii leo na inaelezwa kuwa kufikia sasa wanakubaliana juu ya tarehe hizo.

Bado kuna jumla ya mechi 92 ambazo zinahitaji kuchezwa na vilabu vyote 20.

Ligi ya EPL ilisimamishwa kwa muda usiojulikana Machi 13 kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Siku ambayo ligi itarejea itakuwa ni kilele cha siku 100 kamili toka mechi yake ya mwisho ambapo Leicester City iliitandika 4-0 Aston Villa.

Tofauti kubwa ya hapo awali na sasa ni kuwa ligi hiyo itarejea bila kuwa na mashabiki uwanjani.

arsenal.vs.manchester.united

Jana Jumatano, klabu zote zinazoshiriki EPL zilipiga kura ya kukubali kuanza mazoezi ya wachezaji kugusana. Hiyo ni hatua ya pili baada ya mazoezi binafsi kuanza toka juma lililopita.

Kufikia sasa watu 12 (wakiwemo wachezaji na maafisa wa timu) wamekutwa na maambukizi baada ya watu 2,752 wanaohusika moja kwa moja na ligi hiyo kupimwa afya zao.

Wachezaji na maafisa wataendelea kupimwa mara mbili kwa wiki. Wale ambao watakutwa na maambukizi watatakiwa kujitenga na wenzao kwa muda wa siku saba.

Mipango inayofuata kwa sasa ni kuidhinisha mazoezi ya pamoja na kawaida kwa klabu kujifua na michezo ya ushindani.

Klabu ya Liverpool ipo kileleni mwa ligi hiyo kwa utofauti wa alama 25 huku ikihitaji kushinda mchezo mmoja tu ili kutawazwa kuwa mabingwa.

Kwa upande wa pili wa ligi, klabu za Bournemouth, Aston Villa na Norwich City zipo mkiani na katika hatari ya kushuka daraja.

BBC

Photo Credits: File

Read More:

Comments

comments