Maafisa wa Tume ya huduma za Ushuru wazuru kituo cha kuwaokoa wasichana

KRA
KRA
Maafisa wa Tume ya huduma za Ushuru katika kaunti ya Narok (TSO) walizuru kituo cha kuwaokoa wasichana cha Tasaru katika kipindi cha  kifedha cha mwaka huu.

Lengo kuu la ziara hiyo ilikuwa ni kujumuika na jamii, kutoa msaada pamoja na ushauri nasaha kwa wasichana waliokabiliwa na dhuluma za kijinsia.

Mbali na kuwapa msaada, Narok TSO iliwaelimisha wasichana hao kuhusu athari za ukeketaji kwa afya pamoja na ndoa za mapema.

Pia jamii ilihamasishwa kuhusu umuhimu wa kuwaelimisha watoto wasichana sawia na wavulana.

Isitoshe Narok TSO ilichukua jukumu la kuwahamasisha jamii kuhusu kuacha mila potovu iliyo na madhara na kuwarai kuendeleza mila inayojenga na yenye hadhi katika jamii.

Wasichana katika kituo cha Tasara walielimishwa kuhusu haki zao na jinsi ya kuzipigania watakapotoka na kujiunga na wenzao katika jamii.

Tume ya Narok TSO ilichukua hatua ya kuhamasisha jamii  ya Maasai kuhusu umuhimu wa kumthamini mtoto msichana na manufaa katika mustakabali wake.

Aidha tume  ilitoa msaada wa mahitaji maalum kwa wasichana hao.

Iliwapa chakula kama vile mchele, sukari, mafuta ya kupikia, unga wa mahindi, shashi pamoja na sodo miongoni mwa bidhaa ninyngine.

Kulingana na takwimu za kidemografia na afya, zaidi ya asilimia 40 ya wanawake walio na umri wa kati ya 15 na 19 wanadhulumia kingono. Na yaliyoathiriwa sana ni maeneo kame na jamii ambazo bado zinashikilia itakadi  na utamaduni potovu.

Tasaru ni kituo cha jamii kilichoko Narok na kilianzishwa mnamo 2002, nia kuu ni kuwaokoa wasichana dhidi ya ndoa za mapema pamoja na ukeketaji pamoja na kuwapa elimu.

Jamii ya wafugaji ya Maasai ni miongoni mwa jamii zilizorodheshwa kutekeleza mila potovu ambayo pia ni hatari ya afya.

Kinyume na ilivyo wavulana, wasichana katika eneo hilo  hawajatambuliwa na jamii. Ni wanaume tu pekee wanaopewa kipau mbele katika masuala ya elimu, urithi wa mali na hata kuwa na usemi katika  jamii.

Wasichana wametelekezwa, na mara nyingi huozwa wakiwa na umri mdogo sana wa kati ya 10-17.

Tasaru imekuwa ikikabiliwa na changomoto zikiwemo uhaba wa fedha na mahitaji mengine ya kimsingi. Ikizingatiwa kwamba idadi ya wasichana wanaotorokea kituo hicho huongezeka kila uchao.