Mabwenyenye na wandani wa Uhuru kumfurusha Ruto Mt. Kenya

NA JAMES MBAKA

Wanasiasa na mabwenyenye kutoka ngome ya Rais Uhuru Kenyatta eneo la Mlima Kenya wameungana kudidimiza umaarufu wa naibu rais Wiliam Ruto katika eneo hilo.

Ruto alikuwa anatarajia kupata uungwaji mkono kutoka eneo hilo katika azimio lake la kuwa rais wa Kenya, lakini wanaompinga wanadai kwamba amekuwa akihujumu ajenda ya rais Kenyatta. Wanasema kwamba hafai kushikilia wadhifa huo.

Wapinzani wa naibu rais chini ya mwavuli wa kieleweke sasa wameungana na wafanyibiashara wenye ushawishi kwa lengo la kusambaratisha umaafufu wa Ruto katika ngome ya rais Kenyatta.

Wafanyibiashara hao maarufu siku ya Jumatatu usiku waliandaa kikao na wanasiasa wanaomuunga mkono Uhuru katika hoteli ya Safari Park na kuafikia azimio kwamba “Nyumba ya Mumbi lazima” iunde serikali ijayo.

Wameapa kutumia raslimali zao kupitia ushirikiano baina ya rais Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kusambaratisha mipango ya Ruto katika eneo la Milima Kenya.  Mkutano huu unajiri wakati eneo hilo linajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa BBI mjini Meru siku ya Jumamosi huku kiongozi wa ODM akiwa mgeni wa heshima.

"Tumesikia wale wanaosema BBI ni kupoteza tu muda. Ikiwa ni kupoteza muda basi usije katika uwanja wa Kinoru kupoteza muda. Tafadhali salia nyumbani," Gavana wa Meru Kiraitu Murungi alisema.

Hili likuwa kama onyo kwa wanasiasa wanaompigia debe William Ruto ambao walionekana kutaka kusambaratisha mikutano ya BBI katika maeneo ya Kitui na Narok. Kiraitu alizungumza baada ya kufanya mkutano na Raila katika afisi yake ya Capitol Hill, mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa kisiasa kutoka kanda hiyo.

Awali ilikuwa imetarajiwa kwamba Ruto atakuwa mgeni wa heshima katika mkutano huo lakini Kiraitu ametangaza kwamba mgeni wa heshima atakuwa Raila Odinga. Karibu magavana wote kutoka eneo la Mlima Kenya walihudhuria mkutano huo.

Kiraitu aliandamana na magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Martin Wambora (Embu), Francis Kimemia (Nyandarua) na Muthomi Njuki (Thara Nithi). Nyuki awali alikuwa mwendani wa naibu rais William Ruto.

Mkutano wa Safari Park uliongozwa na mfanyibiashara mashuhuri nchini Peter Munga.