Madaktari wasambaza picha za mapafu meusi ya mvutaji sigara kwa miaka 30

mapafu meusi
mapafu meusi

Kanda ya video ya mapafu meusi yaliyoathirika ya mwanaume wa umri wa miaka 52 inatumiwa kama tahadhari kuhusu madhara ya uvutaji sigara.

Mwanaume huyo anasemekana kuvuta pakiti moja kila siku ya sigara kwa kipindi cha miaka 30.

Video hiyo ambayo imesambaa na kufikia zaidi ya watu milioni 30 imetumika kama onyo kuhusu madhara yanayoletwa na uvutaji sigara.

Kulingana na jarida la Daily Mail, mwanaume huyo alikuwa amesaini kuwa viungo vyake vipewe wagonjwa wengine kuwafaidi.

Hata hivyo madaktari walikataa wito huo wakisema kwamba mapafu hayo si salama kwa binadamu mwingine.

Daktari Chen, kutoka Hospitali ya Wuxi People's Hospital in Jiangsu, Uchina, mpasuaji wa mapafu aliongoza oparesheni hiyo.

Kanda ya hiyo ya video ilionesha mapafu meusi kama makaa, yalioathiriwa na tumbaku kwa miaka mingi.

Aidha, iliwekwa kwenye mtando wa hospitali huku ukiandikwa: "Bado una ujasiri wa kuendelea kuvuta sigara?"

Uvutaji wa sigara ni mojawapo wa uraibu unaoweza kudhibitiwa na ambao husababaisha zaidi ya maradhi 15 mwilini.

Takwimu zinaonesha kwamba  uvutaji sigara husababisha asilimia 70 ya visa vya kansa ya mapafu, kile ambacho wanasayansi wanasema ni kubwa mno ikilinganishwa na aina yoyote ile ya kansa yoyote.

Aidha ripoti hizo huonesha kwamba zaidi watu milioni 1.2 hufariki kila mwaka, huku walio na uraibu huo wakikadiriwa kuwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo.