Madereva 15 wa Kenya wamezuiwa kuingia nchini Uganda kwa sababu ya COVID 19. 15 hao walipatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa katika eneo la Malaba, Busia na hawakuruhusiwa kuingia Uganda.
Ni miongoni mwa raia 19 wa kigeni wakiwemo watanzania wawili na raia wawili wa DRC waliopatikana na ugonjwa huo katika kituo hicho cha mpakani.
" Kuingia kwao nchini Uganda hakujaruhusiwa" taarifa kutoka mamlaka za Uganda imesema.
Uganda imesema matokeo ya vipimo vyao vilivyofanywa Julai tarehe 14 vimethibitisha visa vitatu zaidi vya ugonjwa huo.
Kati ya visa hivyo vitatu, viwili ni vya raia wa Uganda waliowasili kutoka Kenya katika mpaka wa Busia ilhali kisa kingine ni kutokea Kampala. Uganda hadi kufikia sasa ina visa 1,043.
Mwezi Mei waziri wa afya Uganda alipunguza idadi ya walio na virusi hivyo baada ya rais Yoweri Museveni kuagiza kuondolewa kutoka orodha hiyo kwa madereva wote wa kigeni waliopatikana na ugonjwa huo .