Hatari:Magaidi wana njama ya kuishambulia Hoteli kubwa Nairobi-Ubalozi wa Amerika .

Kyle Mccarter
Kyle Mccarter
Marekani imeonya kwamba  magaidi huenda wana njama ya kuishambulia hoteli moja  kubwa jijini Nairobi .

Ubalozi wa Amerika ,Nairobi  umesema  hoteli inayolengwa haijatambuliwa lakini ni mojawapo ya zinazopendwa na raia wa kigeni na wasafiri wanaokuja Kenya kwa biashara .

" Unafaa kuwa mwangalifu unapotembelea hoteli za Nairobi ,fahamu mazingira yako,Tathmini mikakati yako ya usalama na ufahamu utaratibu wa kuondoka katika eneo lolote wakati panapotokea dharura’ imesema sehemu ya ilani hiyo. Kulingana na msemaji wa Ubalozi huo Kenya na Marekani  zinafanya kazi kwa ushirikiano ili kuchunguza hali ilivyo nchini . Ubalozi wa Amerika umesema ilani kama hizo zinawapa habari raia wake ili wafanye maamuzi yafaayo katika mipango yao ya usafiri . Ilani hiyo imejiri huku Inspketa mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai akiwahakikishia wakenya kwamba idara yake ipo katika hali ya tahadhari ili kuwapa ulinzi .

Amesema polisi wameimarisha doria  katika mipaka ya kuingia Kenya na wahalifu wenye nia ya kusababisha usumbufu watazuiawa kuingia nchini .

" Hata hivyo tungependa kuwatahadharisha wananchi kuwa makini zaidi hata polisi na vyombo vya usalama  vinapoendelea na jitihada za kuwahakikishia  usalama wao’ amesema Mutyambai kupitia taarifa .