Magufuli na Kenyatta wazungumza kuhusiana na mgogoro mipakani

Rais Kenyatta na mwenzake wa Tanzania John Magufuli walifanya mazungumzo ili kubaini njia mwafaka ya kutafuta suluhu katika mgogoro ambao umekuwepo kwenye mipaka ya mataifa hayo mawili tangu virusi hatari vya corona kuripotiwa katika mataifa mawili.

Viongozi hao wawili wamekubali wizara zote mbili za usafiri kukutana na kufanya mazungumzo ili kubaini namna shughuli hiyo itakavyoendeshwa kwenye mipaka ya Kenya na Tanzania huku mjadala kuu ukiwa ni kuhusiana na madereva wengi wanaotokea taifa jirani la Tanzania wakiwa wameambukizwa na virusi hivyo.

Katika video na ambayo tumeiona, Magufuli amesema vita vya mipaka ambavyo vimekuwepo vitayawezesha mataifa hayo mawili kuendelea kushirikiana kiuchumi.

"Haiwezekani tukawakwamisha waliokuja kufanya biashara. Lakini pia magari ya Tanzania hayawezi yakakwamishwa kwenda Kenya," alisema Magufuli.

Ameongeza kuwa ni sharti asasi kuu kutoka mataifa husika kuzungumza ili kupata njia mwafaka.

"Wazingatie uchumi wa nchi zetu. Kwa vile tumezungumza vizuri na Kenyatta, sisi tumeyamaliza. Wakae viongozi watatue hii maneno na watu wafanye biashara katika pande zote mbili," amesema Magufuli.

Jumapili, Tanzania ilisitisha shughuli za usafiri wa madereva wa Kenya kuingia nchini humo siku moja tu baada ya rais Kenyatta kufunga mipaka yake na taifa hilo ili kusitisha maambukizi ya virusi hivyo.