Mahakama kutoa uamuzi kuhusu ombi la dhamana la gavana Muthomi Njuki

Mahakama hivi leo Jumanne inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi la gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki kutaka kuachiliwa dhamana.

Gvana huyo ambaye alijisalimisha kwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC siku ya Jumatatu alilazimika kulala ndani ya seli za EACC kwa siku ya pili mfululizo huku akisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu ombi la dhamana.

Njuki na washtakiwa wengine 20 walifikishwa mbele ya mahakama ya Milimani kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa shilingi millioni 34.9 pesa za umma.

Gavana huyo alikanusha mashtaka yote kumi na sita dhidi yake. DPP aliomba mahakama kupuuzilia mbali ombi la washukiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji aliagiza kukamatwa na kushtakiwa kwa gavana huyo na maafisa wengine wa kaunti kuhusiana na utoaji wa zabuni ya shilingi milioni 34.9.

Zabuni hiyo ilikuwa ya kuwekwa mtambo wa kuchoma taka.

Gavana Njuki alishtakiwa pamoja na Fridah Murungi- afisa mkuu wa mazingira, Floridah Kiende- kaimu mkurugenzi wa ununuzi bidhaa, Highton Murithi- afisa wa hazina, Teresia Kagoji- Afisa wa fedha, Arch Lee Mwenda- idara ya barabara, Japhet Mutugi- afisa wa ununuzi bidhaa, Emily Nkatha- afisa wa ununuzi bidhaa na Mike Mwiandi – mhasibu.

Wengine ni Elosy Kariithi, Kenneth Mucuiya, Caroline Wambui, David Mbugua, Margaret Muthoni, Allan Murithi, Japheth Gitonga na George Miano.

DPP alisema kwamba ufisadi huo ulitekelezwa na maafisa wa kaunti katika idara ya utoaji zabuni na fedha waliyopuuza sheria za ununuzi bidhaa.

Soma habari zaidi hapa;

-

-