Maisha ya huntha! changamoto za kuwa na sehemu mbili za siri

Katika kitengo cha Ilikuaje na Massawe Japanni, Kwamboka alijitokeza na kusema waziwazi  vile maisha yake yalikuwa magumu  alipokuwa mchanga kabla ya kukubali mambo yalivyokuwa.

Kwamboka alisema kuwa, wazazi wake walikataa kutimiza wajibu wao  na hata kumwambia ajue atakavyojisaidia.

Visa vya  wazazi kukataa kutimiza wajibu wao kwa watoto waliozaliwa huntha ni vingi sana lakini Kwamboka anatupa moyo leo kutuonyesha kuwa yote yanawezekana.

Kwamboka alisema, alipokuwa mdogo alijaribu kumwambia mamake lakini alikuwa akimchapa kila wakati alipomueleza kuhusu jambo hili na kushindwa ni yupi angemsaidia.

Hivyo basi, Kwamboka alisafiri mpaka Nairobi huku akidhani kuwa atafika na maisha yatakuwa mazuri lakini alipofika Nairobi, mambo hayakuwa alivyotarajia.

Kwamboka alipofika Nairobi alishindwa kujikimu maishani na hapo ikambidi awe chokora.

Baada ya siku nyingi za kuteseka jijini, alikutana na mama mmoja ambaye alikuwa huntha pia na huyo mama akaamua kumchukua na kumpeleka shuleni ambapo alikubaliwa na kupendwa.

Mwenzake Kwamboka  pia alisema kuwa maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wake,  mamake alikuwa anampenda lakini watu wa kwao hawakumkubali.

Cha kusikitisha ni kuwa, mama yake alikuwa anaficha chakula na kumpelekea kwa sababu hakuwa anataka aonekane na watu wengine kwani  ingekuwa tatizo kubwa katika jamii yake.

Vilevile  alisema, maisha  yake shuleni ni magumu kwani ikiwa yuko katika hedhi yeye hupata damu nyingi sana.

Zaidi ya hayo, walisema kuwa kushiriki tendo la ndoa ni changamoto kwake kwani huwa anaogopa kuwa mpenzi wake anaweza kuona na kushtuka ama kumwacha.

Amini usiamini Kwamboka alisema kuwa yeye ana mke na anampenda sana kwani alimkubali alivyo.