‘Majambazi wa genge nilokuwa nikiongoza walimbaka dadangu, najutia usiku huo wa uhalifu’

gangstar 1
gangstar 1
Elvis Chege* alikuwa jambazi sugu na makao yake  yalikuwa mtaa wa Mathare ambako alijulikana kama Escobar ambapo wengi walifahamu shughuli zake za uhalifu na walimuogopa.

Elvis alikuwa na mtandao mkubwa wa usaidizi na hata baadhi ya maafisa wa polisi walifahamika kumsaidia katika kutekeleza uhalifu. Alikuwa na kikosi chake cha  majambazi waliowahangaisha watu katika maeneo mbalimbali ya jiji kati ya mwaka wa  2008 na 2014.  Kilele cha uhalifu wao kilifika mwaka wa 2013 ambapo baadhi ya wanachama wa genge lake walipokamatwa na karibu nusu yao kuuawa katika makabiliano na polisi.

Elvis anajitetea kwamba hali ya umaskini na kukosa ajira ndio iliowafanya kujiingiza katika uhalifu lakini kilichotokea Agosti mwaka wa 2014 kilimfanya kujisalimisha kwa polisi na kuachana na uhalifu kabisa.

Kabla ya kuanza kuwaibia watu kimabavu na hata kuwapiga wengine risasi, Elvis na genge lake walikuwa wakitumia dawa za kulevya, nyingine za kujidunga ili kuweza kujizuia kuhisi huruma  na kustahimili makali ya baridi na hatari ya kuhudumu nyakati za usiku. Siku moja walivamia kituo kimoja cha petroli katika eneo la Muthaiga  na baada ya kuwazidi nguvu wahudumu wa kituo hicho, walichukua pesa zote na kuvunja kamera za cctv katika eneo hilo.  Bila kujua kilichokuwa kikifanyika upande wa pili wa kituo hicho, baadhi ya wanachama wa Genge la Elvis walikuwa wakimbaka mfanyikazi mmoja wa kike wa kituo hicho cha mafuta. Elvis,  kwa sababu ya dawa za kulevya alizokuwa ametumia hakujua kilichokuwa kikifanyika lakini anakumbuka usiku huo walikuwa wametekeleza wizi katika maeneo mawili na kituo hicho kilikuwa cha tatu.

Genge lake lilikuwa limechoka na kuanza kufanya utepetevu kwa hivyo hawakugundua jinsi walivyokuwa wanajikokota kuondoka  eneo hilo. Keshoye asubuhi wakati walipopata  fahamu na kuanza kutathmini kiasi cha pesa walizopora, ndipo Elvis akapigiwa simu na mamake kwamba dadake alikuwa amebakwa na majambazi katika kituo cha petrol. Hakuhitaji kuwa mwerevu kugundua kwamba ni genge lake ndilo lililohusika na wizi na ubakaji wa dadake usiku uliotanguliwa.

Elvis alipowauliza  wanachama wa genge lake iwapo kuna aliyefanya ubakaji, watatu walikiri kumfanyia msichana mmoja ukatili huo na papo hapo Elvis aliitoa bastola yake na kuwaua. Wengine walishangaa kilichofanyika na walipogundua kwamba aliyebakwa alikuwa  dadake kiongozi wao, wengine walitoroka na kujisamilisha kwa polisi. Hapo ndipo masaibu yake yalipoanzia kwani kando na kujutia ukatili ambao dadake alifanyiwa na genge lake. Elvis sasa alikuwa amewekwa katika orodha ya wahalifu sugu wanaosakawa na serikali. Polisi walitundika picha zake magezetini na zawadi ya shilingi milioni moja kuahidiwa kwa atakayetoa habari za kukamatwa kwake.

Maisha ya kukimbilia maisha yake na  majuto ya ukatili uliotendewa dadake yalimfanya Elvis kujisalimisha kwa polisi kupitia shirika moja la kutetea haki za binadamu. Alishtakiwa na hata kuthibitisha akiwa jela kuwa amebadilika lakini baada ya kuachiliwa, Elvis yungali na machungu na majuto ya jinsi uhalifu wake ulivyoyaathiri maisha ya dadake wa toka nitoke.