Malimwengu haya! Jamaa amzika kuku na kusoma bibilia kaburini mwake

lugari.000.chicken
lugari.000.chicken

Ninaamimi kuwa sote tunajua kuku kama mnyama anayetupa mayai na ndege ambaye tunaeza mla endapo amefariki.

Hata hivyo, sivyo kwa Joseph Omulai kwani kuku wa jamaa huyu alikufa na badala ya kumla kama desturi ya wengi, akaamua kumzika kuku wake.

Joseph Omulai kutoka kitongoji cha maji mazuri kaunti ya Lugari, alifanya mazishi ya kuku ambaye alikuwa amempenda sana na hata kusema kuwa atafanya misa ya ukumbusho wa ndege wake.

Majirani waliitwa na nyimbo za kuomboleza za Joseph Omulai. Wengi walishangaa sana baada ya kufika nyumbani kwake na kuskia kuwa, Joseph alikuwa anaomboleza kifo cha kuku wake ambaye alisema kuwa, alikuwa ameyalalia mayai 12 ambayo yalikuwa yatage kwa wiki mbili.

Omulai alichimba shimo ya mita tatu jumamosi na kuwa na misa ya mtu mmoja huku akisoma bibilia na kuomba. Alimfunika kuku wake na kitambaa cheupe na kumzika.

Kwenye Kaburi, aliandika Rass Hen 2019.

Omulai alisema kuwa alimpenda sana kuku wake na kifo chake kilimsikitisha sana. Vilevile, alisema kuwa kuku huyu alifariki baada ya kugongwa na mwanakijiji na aksema kuwa, badala ya kumtupa aliona ni vyema amzike.

''Nilikuwa nimenunua vifaranga saba mwaka uliopita nikawalinda lakini bahati mbaya wengine wakaibiwa na nikabaki na huyu mmoja ambaye nilikuwa nangoja mayai yake yatage. Lakini mtu alimgonga kuku wangu na kusababisha kifo chake.'' Omulai alisema.

Mwanakijiji Halima Daraja alisema,

''Niliambiwa kisa hiki na jirani yangu lakini sikuamini na nilipokuja hapa, nilipigwa na butwa kufika na kuona ni ukweli Omulai anaomboleza kuku. ''

Jirani mwengine alisema kuwa, aliambiwa ujumbe huu na watoto wake na hakuamini na hata kuwaambia watoto wake waache uongo.

''Watoto wangu nao waliniambia niende nijionee mwenyewe na nilipofika, sikuamini niliyoyaona.''Alisema.

Caroline Awinja alisema hakuweza kushuhudia mazishi ya kuku huyo lakini atafanya juu chini awe katika misa ya ukumbusho wa kuku huyu.

Ama kwa hakika, ukistajabu ya Musa, utayaona ya Firauni.