Kilonzo anasema katika jamii yake, mama mkwe ni mtu wa heshima sana na kuna vitu ambavyo hafai hata kuvifanya. Baada ya kuwa na mke wake kwa miaka mitano alitaraji kwamba mama mkwe ataweza kuwacha waishi maisha yao bila usumbufu wake.
Lakini unajiuliza ni usumbufu upi huu? Mama mkwe wake Kilonzo amekuwa akimkonyezea jicho ! Kilonzo haelewi mbona lakini anasema wakati mmoja mkewe hakuwa nyumbani na mama mkwe ndiye aliyekuwa ameachwa na watoto. Miongoni mwa majukumu yake siku hiyo ilikuwa kuwatayarishia watoto chakula cha mchana lakini mama mtu aliamua kuitumia fursa hiyo kujaribu kufanya kitendo kisichoweza kutarajiwa kutoka kwa mama mkwe.
‘Aliponiletea chakula, alinipa maji ya kunawa mikono kisha akanikaribia akitaka kunikalia miguuni. Nilishtushwa na kitendo hicho na kumskuma kando. Nilishangaa nini kimemwingia lakini hiyo haikuwa mwisho wa majaribio yake’ anasema Kilonzo. Wanapozungumza mama mkwe humuambia vitu vingine kwa mafumbo kuashiria kwamba anachomfanyia mwanawe naye mama mkwe anaweza kukifanya hata bora zaidi.
Kilonzo ameogopa kumuambia mkewe kuhusu tabia za mamake na hilo limemsumbua kwa muda sana. Hataki kuharibu uhusiano kati ya mkewe na mamake na pia kwa sababu wajukuu zake wanampenda sana na mgogoro wowote utakaozuka utawatenganisha na nyanya yao.
Kila wakati mama mkwe anapomuangalia, yeye humfinyia jicho hatua ambayo anasema inavuruga heshima ambayo inafaa kuwepo kati ya mtu na mama mkwe wake . Kilonzo yupo katika njia panda, je amuambie mke wake kuhusu tabia za mamake au anyamaze na aendelee kupitia masaibu haya? Ungefanya nini iwapo ungejipata katika hali hii ya Kilonzo?