Mama wa taifa aishauri jamii kubuni mikakati ya kubadilisha maisha ya vijana

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta leo amewataka Wakenya ikiwemo mashirika ya serikali na yale yasio ya kiserikali kutekeleza mipango inayokusudiwa kuboresha maisha ya vijana na watoto.Alisema mipango ya maendeleo ya kijamii ambayo inasaidia kukuza na kuimarisha vipawa vya watoto yapaswa kustawishwa zaidi kuwafikia watoto na vijana wengi zaidi kote nchini.

 Mama wa Taifa alisema haya leo alipotembelea mpango wa kukuza vipawa vya muziki miongoni mwa watoto na vijana unaotambulika kama Ghetto Classics ulioko kanisa katoliki la St. John’s, mtaa wa Korogocho, katika kaunti ya Nairobi. Ghetto Classics ni mpango wa Wakfu wa Usanii wa Muziki ambao kwanza ulianzishwa katika mtaa wa Korogocho mwaka wa 2009 lakini sasa umesambazwa katika kaunti mbali mbali huku ukinufaisha zaidi ya watoto na vijana wapatao 1,500.

“Elimu ya muziki husaidia kukuza shauku na ubunifu wa watoto wetu na ina uhusiano wa moja kwa moja na ufanisi katika masomo ya watoto wetu,” kaongeza.

Mpango huo unatoa mafunzo ya muziki na usanii kwa zaidi ya watoto 300  katika mtaa wa Korogocho mbali na kuwapa ujuzi wa mbinu za kubadilisha maisha yao na jamii hiyo kwa jumla.Alisema Mpango wa Ghetto Classics umefaulu kuwezesha vijana na watoto kwa kukuza vipawa vyao vya muziki na usanii ili kukabiliana ipasavyo na changamoto za maisha.

“Shughuli zinazotekelezwa katika kituo hiki hutoa fursa kwa kila mtoto kupokea uwezo na ahadi ya elimu, na nafasi ya kunufaika kikamilifu kutokana na talanta zao na kuafikia kilele cha uwezo wao,” kasema Mama wa Taifa.

 “Elimu ya muziki husaidia kukuza shauku na ubunifu wa watoto wetu na ina uhusiano wa moja kwa moja na ufanisi katika masomo ya watoto wetu,” kaongeza.

Mama wa Taifa ambaye aliandamana na Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohamed alipongeza mradi wa watoto na vijana wa Mpango wa Ghetto Classics akisema unaleta manufaa mengi zaidi ya kukuza vipawa vya usanii kama vile kukuza ujasiri, nidhamu na moyo wa ushirikiano.

“Mradi huu pia unahusika na kuwapa vijana uwezo wa kuwa wanasihi na kielelezo kwa wengine – wengi wenu mmekuwa watu wa kuleta mabadiliko katika familia na jamii zenu,” Mama wa Taifa aliwaambia mamia ya vijana hao.

Aliwahimiza waanzilishi wa mradi huu kusajili watoto na vijana zaidi akisema utawasaidia kuwaepusha vijana wanaobalehe  na maovu ya kijamii na kuwaelekeza katika njia sawa ya maisha.

“Natambua kuna mengi ya kuwavuruga wavulana wanaobalehe ikiwemo ushawishi wa kuacha masomo ili kutafuta hela. Na wasichana wengi wanaendelea kushinikizwa kuingia ndoa za mapema na kuwa akina mama na hivyo kuachwa nyuma,” kasema Mama wa Taifa.

Alipongeza Parokia ya Kanisa Katoliki ya Kariobangi na jamii ya Korogocho kwa kuandaa mpango huo akidokeza kwamba umekuwa sehemu muhimu ya jamii.

 Balozi Mohammed alipongeza watoto na vijana wa Korogocho kwa kuchagua kubadilisha maisha yao kwa kuwa sehemu ya Mpango wa Ghetto Classics. Alipongeza wazazi wa walionufaika na washikadau kwa kushirikiana kuanzisha mpango huo mkubwa akisema umewapa vijana katika eneo hilo nafasi ya kubadilisha maisha yao.

“Mwanzo wako huwezi ukabainisha siku zako za baadaye. Tunabainisha siku zetu za baadaye licha ya mwanzo tulio nao. Sote tunapata nafasi ya kubainisha siku zetu za baadaye," kasema Waziri wa Michezo.

 Elizabeth Njoroge ambaye ni mwazilishi wa mpango huo alisema Ghetto Classics ilitokana na haja ya kufungua nafasi kwa watoto na vijana kutoka familia ambazo hazijabahatika kuboresha muziki wao na talanta.

Alitambua changamoto za Mama wa Taifa za kuendeleza mpango huo  zaidi na akatoa wito wa ufadhili zaidi kutoka kwa washikadau  na wahisani kuwalinda watoto wanaoendelea kuongezaka na vijana walio na nia ya kujiunga na mpango huo. Wengine waliozungumza kwenye hafla hiyo walikuwa Mwenyekiti wa Wakfu wa Safaricom Joseph Ogutu na Padri wa Parokia ya Kanisa Katoliki ya Kariobangi Andrew Wanjohi.