Mama wa taifa wa Burundi alazwa nchini baada ya kupatikana na virusi vya corona

Burundi-First-Lady
Burundi-First-Lady
Denise Bucumi Nkurunziza, mama wa taifa la Burundi kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan Nairobi baada ya kuripotiwa kuwa ameambukizwa virusi vya corona.

Taarifa zinasema kuwa Bucumi alisafirishwa kwa ndege kutoka mji mkuu wa Bujumbura Alhamisi asubuhi akiwa kwa ndege ya shirika la AMREF.

Taarifa kuhusiana na hali yake kwa sasa bado haijabainika.

Mumewe Pierre Nkurunzinza hakuwa katika ndege hiyo japo alikuwa na walinzi watatu ambapo mmoja kati yao pia alipatikana na virusi hivyo.

Haijabainika wazi ni vipi alivyoruhusiwa kuingia nchini huku shughuli za ndege katika taifa la Kenya zikiwa zimesitishwa kwa sasa.

Nkurunzinza amekuwa akikashifiwa kuhusiana na hatua ambazo alikuwa ameweka kwa taifa hilo ili kukabiliana na virusi hivyo hatari.

Mapema mwezi huu, taifa la Burundi liliwafukuza wakuu wa shirika la afya duniani ambao walikuwa wanaangazia namna taifa hilo lilikuwa linaendesha shughuli za kuwapima wananchi wake.

Kufikia sasa, ni taifa la kipekee katika bara la Afrika ambalo halikusitisha kamwe ligi kuu ya nchini humo.

Kwa sasa, taifa hilo linaendelea kusubiri hatima ya iwapo matokea ya uchaguzi mkuu uliokuwa unafanyika yatakubalika na mahakama baada ya kiongozi wa upinzabni kudai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na uongo mwingi.

Jenerali Evariste Ndayishimiye kutoka kwa chama tawala alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 60 ya kura zilizokuwa zimepigwa.