Man United wakubaliana mkataba wa kumsajili Bruno Fernandes

bruno fernandes
bruno fernandes
Manchester United wamekubaliana mkataba wa kumsajili kiungo wa kati wa Ureno Bruno Fernandes kutoka Sporting Lisbon.

United watalipa kitita cha kwanza cha takriban Uro milioni 55 kwa mchezaji huyo wa miaka 25, ingawaje marupurupu huenda yakafanya kitita hicho kufikia Uro milioni 80.

Uhamisho wa Fernandes utakamilika baada ya uchunguzi wa kimatibabu na masuala mengine ya kibinafsi. Vilabu hivyo vimekua vikijadiliana wakati wote wa dirisha la uhamisho huku makubaliano yakiafikiwa Jumanne.

Mkusanyiko wa habari za spoti

Mohamed Salah alikuwa nyota wa mechi Liverpool walipoongeza uongozi wao kileleni mwa jedwali la ligi ya Primia kwa alama 19 baada ya kuwanyuka West Ham 2-0. Salah alianza kufunga kunako kipindi cha kwanza kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain kuongeza bao la pili.

Vijana wa Jurgen Klopp sasa wamewanyuka wapinzani wao wote wa ligi angalau mara moja msimu huu. Ushindi huo unawawacha West Ham katika nafasi ya 17 kwenye jedwali.

Manchester City walifuzu kwa fainali ya kombe la Carabao licha ya kupoteza 1-0 katika mkondo wa pili wa nusu fainali kwa Manchester United.  Ilionekana kama itakuwa rahisi kwa City baada ya kushinda mkondo wa kwanza 3-1 ugani Old Trafford wiki tatu zilizopita, lakini bao la Nemanja Matic kunako kipindi cha kwanza likabadilisha mambo.

City walikosa nafasi nzuri katika kipindi cha pili lakini jitihada zao za kufika fainali ya mashindano hayo zilipigwa jeki baada ya Matic kupewa kadi nyekundu na kuwawacha United na wachezaji 10.

Arsenal haitakubali kumuuza mshambuliaji wao raia wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang mwenye umri wa miaka 30, kwa dau la chini ya pauni milioni 50.

Barcelona inaripotiwa kumnyatia mshambuliaji huyo. Kwingineko Sheffield United ndiyo klabu pekee ambayo imepeleka ofa ya usajili kwa kiungo wa klabu ya Genk na taifa la Norway Sander Berge ambaye ana thamani ya pauni milioni 27.

Mashindano ya riadha ya dunia mwaka 2020 ambayo hufanyika ukumbini huko Nanjing yameahirishwa, kutokana na hofu ya kusambaa kwa virusi vya coronavirus nchini Uchina.

Mashindano hayo yalikuwa yafanyike kuanzia Machi tarehe 13 hadi 15 lakini bodi ya usimamizi wa riadha duniani ikaiahirisha kwa miezi 12. Bodi hio ilitafuta ushauri kutoka kwa shirika la afya duniani na kukataa ofa kutoka kwa miji mingine.

Mabingwa watetezi Gor Mahia walifungua mwanya wa alama mbili kileleni mwa jedwali la KPL baada ya kupata ushindi 2-1 dhidi ya Sofapaka jana mjini Kisumu. Mechi hio ilipelekea Gor, ambao wana mechi moja mkononi kumuanzisha mchezaji wao mpya waliomsajili raia wa Uganda Juma Balinya, ambaye mchango wake ulimpelekea kusifiwa na kocha Steven Polack.

Lawrence Juma na Kenneth Muguna walifungia Gor huku Jedinal Ameyaw akiwapa Sofapaka bao lao.

Waogeleaji wa Kenya wanapowania kuiwakilisha nchi katika mashindano jijini Tokyo wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya kamati ya kitaifa ya Olimpiki kufichua kuwa malumbano yanayolikumba shirikisho lao, hayataathiri kushiriki kwao. Waogeleaji hao walikua wako katika hatari ya kufungiwa nje ya Olimpiki baada ya shirikisho la Kenya kupigwa marufuku na lile la kimataifa la uogeleaji kwa kukosa kulainisha masuala yao.

Kenya tayari imewataja waogeleaji wanne kushiriki mashindano hayo. Ni pamoja na Emily Muteti, Issa Abdulla, Danilo Rosafio na Maria Brun-lehner.