Manchester United yashindwa kutamba nyumbani

Sare ya bao moja dhidi ya mahasimu Arsenal ilimaanisha kuwa Manchester United wamesajili mwanzo mbovu zaidi katika ligi ya primia nchini Uingereza kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Katika kabiliano lililokuwa kivuli cha ubabe wa timu hizo mbili miaka ya nyuma, Scott McTominay aliweka Manchester United kifua mbele dakika za mazidadi kipindi cha kwanza kwa kombora zito lililomuacha mlinda lango wa Arsenal Bernd Leno kinywa wazi.

Arsenal ilisawazisha mambo kupitia nyota wao matata Pierre-Emerick Aubameyang aliyedengua safu ya ulinzi ya Manchester United na kumuacha mlinda lango David Degea akiwa ameinua mikono kana kwamba anaswali.

Awali bao la Aubameyang lilikuwa limekataliwa na msaidizi wa refa lakini VAR ikabatilisha uamuzi huo baada ya video kuonyesha kuwa Aubameyang hakuwa ameotea kwa hisani ya Harry Maguire.

Mlinda lango wa Arsenal Bernd Leno alikuwa kisiki kwa mashambulizi ya Manchester United huku akipangua mikiki ya Maguire na Marcus Rashford.

Chipukizi wa Arsenal Bukayo Saka nusra aweke The Gunners kifua mbele lakini komboro lake lilimgonga Victor Lindelof na kupaa juu ya mtambaa panya.

McTominay pia alipiga kichwa maridadi lakini hakulenga shabaha baada ya kona iliyochanjwa maridadi na Ashely Young. Baada ya mchuano huo Arsenal imepanda hadi nafasi ya nne katika jedwali la ligi ya primia huku United ikifunga ukurasa wa kumi bora.

Matokeo haya yanamaanisha Manchester United wamesajili matokeo duni zaidi baada ya mechi saba za ligi katika kipindi cha miaka 30 sasa.