Maraga awataka magavana na wabune kuafikiana kuhusu mgao wa kaunti

gov
gov
Jaji mkuu David Maraga kwa mara nyingine tena amewashauri magavana na wabunge kufanya mazungumzo ili kuafikiana kuhusu utata unaozingira mgao wa pesa za kaunti.

Jaji mkuu anasema mahakama ya upeo haingependa kujihusisha na swala hilo.

"Tumekutana leo asubuhi kama majaji wa mahakama ya upeo na tunahisi tusihusishwe katika kutoa uamuzi kuhusu swala hili. Hii ni shughuli ya bunge ambayo inafaa kushughulikiwa kikamilifu na mabunge yote mawili. Lakini kama itabidi basi tutaingilia kati," alisema siku ya Jumanne.

Mswada mpya wa ugavi wa pesa za kaunti utawasilishwa bungeni Jumanne. Mswada mpya unapeondekeza serikali za kaunti kupewa jumla ya shilingi bilioni 316.5, ikiwa utapitishwa bungeni huenda ukakwamua utata uliyoko sasa baina ya seneti na bunge la kitaifa.

Bunge la kitaifa mapema lilikuwa limependekeza mgao wa shilingi bilioni 310 lakini pendekezo hilo halikupata muafaka. Wakili wa bunge la kitaifa aliambia mahakama kuwa mswada huo ulikuwa umeandaliwa na tayari kuwasilishwa bungeni Juma hili.

Maraga aliagiza pande husika kufika mahakamani siku ya Jumatano wiki ijayo ikiwa hawatakuwa wamepata muafaka.