Maraga hakuelewa agizo la rais la mabadiliko serikalini, AG Paul Kihara asema

kihara
kihara
Agizo maalum la rais Uhuru Kenyatta kuhusu mabadiliko katika usimamizi wa serikali halikinzani kwa vyovyote vile na katiba ya Kenya, mwanasheria mkuu Paul Kihara amesema.

Kihara alikuwa akimjibu Jaji mkuu David Maraga aliyedai kwamba rais alikosea kuingilia uhuru wa idara ya mahakama kutokana na agizo hilo jipya la rais.

Soma pia;

Maraga alishtumu hatua ya agizo hilo maalum la rais kujumuisha Tume ya huduma kwa mahakama chini ya idara za serikali ambazo zinawajibikia rais.

Jaji mkuu alisema kwamba Tume ya huduma kwa mahakama iko chini ya mahakama na haiwezi kupewa majukumu na serikali.

lakini katika taarifa yake siku ya Alhamisi mwanasheria mkuu Paul Kihara alisema kwamba Maraga hakupata ufahamu kamili wa agizo hilo la rais.

Soma pia;

"Hakuna kitu katika agizo hilo la rais kinachodhalilisha kitengo au taasisi yoyote ya serikali  au kuchanganya umma," alisema.

Aliongeza kwamba agizo hilo linalenga kubainisha wazi majukumu ya wizara na idara za serikali ukizingatia ushiriakiano wazo.

"Ni jukumu la rais kufafanua majukumu ya idara za serikali na mbinu za kuleta sera ya kuimarisha ushirikiano baina yazo ili kupiga jeki utendakazi wa vitengo vya serikali."  Taarifa ilisema.

Soma pia;

Mwanasheria mkuu alifafanua kwamba hakuna muingilio wowote katika uhuru wa mahakama katika agizo hilo la rais. Alisema kwamba haihujumu kamwe utendakazi wa kitengo hicho huru kama ilivyo katika katiba ya Kenya.

"Hakuna kipengele katika agizo la rais kinacholenga kufanyia mabadiliko idara ya mahakama au kuipa idara hiyo majukumu."Alieleza.

Agizo hilo la Mei 11, linalenga kufanyia mabadiliko usimamizi na shughuli za idara mbalimbali za serikali. Agizo hilo linatupilia mbali lile la Julai mwaka 2018.