Margaret Kenyatta ataka kubuniwa kwa nafasi zaidi za elimu kwa akina mama

margaret kenyatta
margaret kenyatta
Mama wa Taifa Margaret Kenyatta ametoa wito kwa washika dau katika sekta ya elimu nchini kubuni nafasi zaidi za elimu ili kunufaisha wanawake ambao elimu yao imesitishwa kutokana na sababu mbali mbali.

Mama wa Taifa aliyezungumza hapo jana alipoongoza kufunguliwa rasmi kwa Chuo cha WE katika sehemu ya Enelerai katika Kaunti ya Narok alisema kuna haja ya kutafuta suluhisho kwa wasichana na wanawake ambao elimu yao imecheleweshwa au kuvurugwa na vizuizi vya kijamii na kitamaduni.

“Natoa wito kwa sisi sote kudumisha juhudi hizi ili tutafute njia za kuelimisha wasichana na wavulana zaidi; na kutafuta suluhisho kwa wasichana na akina mama ambao elimu yao imecheleweshwa au kuvurugwa,” kasema Mama wa Taifa.

Chuo cha WE ni taasisi ya kipekee inayotoa mafunzo mbali mbali kwa wasichana walioathirika hasa wanaotoka katika jamii ya kuhamahama ya Maasai katika Kaunti ya Narok.

Chuo hicho kinatoa mafunzo katika uuguzi, afya ya umma na utalii na kinajibidiisha kuanzisha mafunzo mapya katika matibabu na upasuaji, afya ya jamii, sayansi ya mahabara na usimamizi wa habari za afya.

Chuo hicho ambacho kimedhaminiwa na shirika la WE Charity kutoka nchini Canada kilianzisha mfumo wa kipekee wa kuwapa vijana mafunzo huku wakisalia karibu na familia zao katika mazingira wanayoyafahamu vyema.

“Elimu huleta faida kubwa zaidi kushinda uekezaji wowote wa kijamii ambao tunaweza kuwapa watoto wetu na kuvunja msururu wa umaskini,” kasema Mama wa Taifa.

-PSCU