Masaibu bado yamzonga Waititu

WAITITU
WAITITU
Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu anakodolea macho tena mashtaka mengine ya ufisadi huku maafisa wa upelelezi wakikaribia kumaliza uchunguzi kuhusu mradi wake uliozingirwa na utata wa Kaa Sober uliogharimu shilingi bilioni moja.

Gazeti la The Star limebaini kuwa tume ya Maadili na kupambana na ufisadi (EACC) tayari imewahoji maafisa wakuu katika utawala wa Waititu, na kuzidisha masaibu ya gavana huyo ambaye tayari anakabiliwa na kesi ya sakata ya shilingi milioni 588. Maafisa wa EACC pia wamezuru wadi kadhaa katika kaunti ya Kiambu, wakiangazia idadi ya walionufaika kutokana na mradi huo.

 Habari zaidi:

Ikiwa kesi ya pili itawasilishwa dhidi ya Waititu itakuwa pigo kwa azma yake kisiasa, gavana huyo ni nguzo muhimu kwa azma ya naibu rais William Ruto kuwa rais katika eneo la kati. Tayari amezuiliwa kuingia afisini mwake huku kesi ya ufisadi dhidi yake ikiendelea.

Jumanne, msemaji wa EACC Yassin Amaro alithibitishia The Star kwamba uchunguzi huo unakaribia kukamilika.

“Watu kadhaa waliokuwa wamehusika moja kwa moja kwa mpango huo walihojiwa. Uchunguzi umepiga hatua muhimu na tuko katika awamu ya mwisho,” Amaro alisema.

Habari zaidi:

Waititu amekuwa akikabiliwa na madai chungu nzima ya ufujaji wa pesa za kaunti na kudaiwa kutumia raslimali hizo kujitajirisha. Uchunguzi wa EACC kwa mfano waonyesha kuwa kiwango fulani cha shilingi milioni 221.5 ambazo tayari zimelipwa katika sakata ya shilingi milioni 588 zililipwa kwa akaunti inayomilikiwa na kampuni ya gavana huyo.

Mradi wa Kaa Sober ulianzishwa Februari mwaka 2018 lakini umekumbwa na utata kuhusiana na idadi ya walionufaika kutokana na mradi huo. Kuna madai kwamba palikuwepo mianya mingi ya kufyonzwa kwa pesa hizo.