Maseneta 20 wanataka kuwa magavana 2022

mgao
mgao
Kivumbi kikali cha kisiasa kinanukia  kwani takriban maseneta 20 wanataka kuwa magavana katika uchaguzi mkuu wa 2022 ili kushikilia nyadhifa hizo zenye mamlaka makubwa na pesa nyingi. Wajumbe hao  wameonyesha nia ya kuwania viti hivyo hadharani  na kutayarisha jukwaa kwa makabiliano makali  miaka miwili tu kabla ya uchaguzi ujao.

Kenya ina maseneta 67 huku 47 wakiwa waliochaguliwa na 20 wakiteuliwa bungeni na vyama mbalimbali. Magavana wana mamlaka zaidi na pia wanasiamia kiasi kikubwa cha raslimali  kuliko maseneta ambao mshahara wao kila mwezi ni takriban shilingi laki sita  pamoja na marupurupu mengine.

Magavana takriban 20 wanahudumia mihula yao ya kwanza huku wengine 21  wakiwa katika mkondo wa lala salama baada ya kuhudumu kipindi cha kwanza.

Miongoni mwa wanaokamilisha hatamu zao ni  mwenyekiti wa baraza la magavana  Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa), Okoth Obado (Migori), Josphat Nanok (Turkana)  na Jackson Mandago (Uasin Gishu).

Maseneta Johnson Sakaja (Nairobi), Fred Outa (Kisumu), Ochillo Ayacko (Migori), Irungu Kang'ata (Murang’a), James Orengo (Siaya)  na  Cleophas Malala (Kakamega)  wote wametangaza nia zao kutaka kuwa magavana .

Wengine ni Steward Madzayo (Kilifi), Ledama Olekina (Narok), Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Aaron Cheruiyot (Kericho), Samson Cherargei (Nandi), Enoch Wambua (Kitui)  na Susan Kihika (Nakuru).

Wengi zaidi hawataki kutangaza nia zao mapema lakini tayari wameanza mikakati ya kujitayarisha kuwania viti hivyo.

Wadadisi wanasema kinachowavutia wengi kutaka kuwa magavana ni mamlaka, ushawishi na raslimali ambazo magavana wanasimamia.

“Pesa na maamlaka  ni vitu viwili vinavyowapa msukumo zaidi . kila mtu anapigania kuingia kuliko na pesa   ,hata katika uchaguzi  mkuu uliopita wachache sana walitaka kuwa maseneta kwa sababu haina fedha  ,maseneta hawasimamii raslimali zozote’ anasema mchanganuzi Martin Andati