Maseneta waliounga mkono ugavi wa mapato wamefungiwa akaunti zao-seneta Aaron Cheruyoit asema

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot amedai serikali imefunga akaunti za benki za wabunge waliopinga hoja ya ugavi wa mapato iliyopendekezwa na Jubilee.

Kulingana na Cheruiyot maseneta wote waliounga mkono hoja ya Seneta Mithika Linturi walishtuka kupata akaunti zao hazifanyi kazi na kwamba Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) inawadai.

Kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii ya twitter, seneta huyo alisema kuwa ni lazima na jukumu la Wakenya kupigana vita dhidi ya ukiukaji wa sheria bila kuchukuliwa hatua.

"Maseneta kadhaa waliounga mkono mswada wa marekebisho kwa mfumo wa ugavi wa mapato ulioandaliwa na Seneta Linturi wamefungiwa akaunti zao na eti KRA nawadai." Aliandika Aaron.

Usemi wake unajiri siku chache baada ya Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang'ata kusema kuwa, wanachama waliokwenda kinyume na msimamo wa chama kuhusu mfumo tata wa ugavi wa mapato wangechukuliwa hatua.

Kwa mara ya nane maseneta Jumanne, Agost 11 kwenye kikao chenye mgogoro, walishindwa kupitisha mfumo wa ugavi wa mapato.

Kutokana na likizo waliyopewa, Wakenya watahitaji kusubiri mwezi mmoja kufahamu kuhusu mswada huo tata wa ugavi wa mapato.

Maseneta chini ya mwavuli wa Team Kenya waliunga mkono mapendekezo ya Linturi yaliyosema kaunti zote 47 zigawane KSh 270 bilioni kwa usawa, badala ya KSh 316.5 bilioni alivyokuwa amependekeza Seneta Johnson Sakaja.