Mashabiki washambulia nyumba ya nahodha wa Sierra Leone kwa kukosa mkwaju wa penalti

sierra leone
sierra leone
Mashabiki waliojawa na ghadhabu wa timu ya taifa ya Sierra Leone wameshambulia nyumba ya mchezaji mmoja baada ya kukosa kufunga mkwaju wa penalti.

Nahodha Umaru Bangura alikosa mkwaju huo katika dakika za lala salama mbele ya mashabiki Jumapili. Hii ina maana kwamba Sierra Leone walikosa kufuzu kwa raundi inayofuata ya michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia la mwaka 2022.

Liberia ilifuzu kwa kushinda jumla ya mabao 3-2. Baada ya mechi hio mashabiki waliirushia mawe nyumba ya Bangura na kuharibu vibaya nyumba yake jijini Freetown.

Hayo yakijiri, Azerbaijan walipata alama yao ya kwanza katika michuano ya kufuzu kwa Euro mwaka 2020 baada ya kutoka sare dhidi ya Croatia katika kundi E, matokeo yaliyowashangaza wengi.

Azerbaijan walikua wamepoteza mechi zao zote nne kufikia sasa lakini bao la kushangaza la Tamkin Khalilzade likawapa matokeo hayo. Dejan Lovren, Ivan Perisich na Marcelo Brozovic wote walikua wameanza upande wa Croatia na kuongoza kupitia bao la Luka Modric kupitia mkwaju wa penalti.

Mlinzi wa Manchester United Diogo Dalot amekua akipokea matibabu nchini Uchina anapojaribu kupona jeraha lake la paja. Inaarifiwa kwamba Dalot aliwasili Shanghai Agosti tarehe 29 na kupokea matibabu maalum kwa siku kumi.

Mchezaji huyo wa miaka 20 raia wa Ureno amekosa mechi zote nne za United walizocheza kufikia sasa msimu huu, huku meneja Ole Gunnar Solskjaer akisema mwezi uliopita kwamba ana matumaini kua ataregea baada ya mapumziko ya kimataifa.

Kwingineko, matumaini ya Northern Ireland ya kufuzu kwa michuano ya Euro mwaka 2020 yalididimia walipopoteza 2-0 kwa Ujerumani katika mechi ya kusisimua uwanjani Windsor Park.

Bao la Marcel Halsten-berg kunako kipindi cha pili na la dakika za mwisho la Serge Gnabry liliwapa vijana wa Joachim Low ushindi. Ujerumani wamepanda hadi kileleni kwa kundi C, juu ya Northern Ireland kwa wingi wa mabao.

Tukirejea nchini, Bandari watazikosa huduma za kiungo wa kati Abdalla Hassan na mshambulizi Yema Mwana wakati wa mechi yao ya mkondo wa kwanza ya kufuzu kwa michuano ya kombe la Caf Confederation dhidi ya Tunisia Ben Guardane uwanjani Kasarani Jumamosi.

Kocha mkuu wa Bandari Bernard Mwalala anasema ni pigo kubwa kuwapoteza wachezahi hao wawili. Mwalala anasema wawili hao walipata majeraha wakati wa mechi za ligi ya Super Cup na KPL dhidi ya Gor Mahia na Mathare United mtawalia.