Mawaziri 2 wapanga njama kumfurusha Maraga, kunani?

Mawaziri wawili wamekuwa wakipanga njama kumuondoa ofisini Jaji Mkuu David Maraga.

Wawili hao walio na uhusiano wa karibu na rais Uhuru Kenyatta, wamefanya mikutano kadhaa kumjadili Maraga na idara ya mahakama.

Katika mkao na wanahabari siku ya Jumatatu, Jaji mkuu aliambia wakenya changamoto anazopitia na kufichua kuwa baadhi ya mawaziri na makatibu wa kudumu wanapanga njama dhidi yake.

Maraga aliyeonekana mwenye gadhabu akihutubia taifa nje ya makao makuu ya mahakama ya upeo jijini Nairobi, alidai kuwepo kwa njama ya kisiri ya serikali kumng’atua ofisini ifikiapo Disemba 31.

“Baadhi ya mawaziri wanasema nitaondoka kabla ya mwihsho wa mwaka. Kumbe hii Kenya ina wenyewe ?" Maraga alisema.

Majaji wa vyeo vya juu walisema siku ya Jumatatu kuwa mawaziri hao wamegadhabishwa na hatua ya Maraga kudinda kukubali kufanya mambo wanavyotaka.

"Walimtaka Maraga kuondoa baadhi ya majaji wanaoonekana kuwa wakaidi kwa serikali na ambao wamekuwa wakitoa maagizo kuzuia miradi ya serikali. Maraga alipokataa walianza kusema kwamba Jaji mkuu ni kikwazo," jaji wa mahakama ya rufaa alisema.

 

 

Mawaziri hao kisha waliagiza maafisa katika ikulu ya rais kutomruhusu Jaji mkuu kukutana na rais. Waliagiza maafisa wa uhamiaji kutoruhusu Maraga na baadhi ya maafisa wakuu katika idara ya mahakama kusafiri nje ya nchi bila idhini ya serikali.

Wawili hao pia walichangia sana katika azimio la kupunguza bajeti ya idara ya mahakama.

Hii si mara ya kwanza kwa jaji mkuu kukabiliwa na njama ya kumuondoa ofisini. Maombi kadhaa yamewasilishwa kwa lengo la kumng’atua afisini Maraga bila mafanikio.

Pia pamekuwepo maombi ya kutaka kuwafurusha majaji Njoki Ndung’u, Smockin Wanjala, Mohamed Ibrahim na Jackton Okwang.

Mwenyekihti wa chama kcha mawakili nchini, tawi la Nairobi Charles Kanjama aligusia maamuzi ya mahakama yalionekana kukwaza sana upande wa serikali kuwa chanzo cha uhasama baina ya mahakama na serikali.

Maraga;pia alisema kwamba amezuiliwa kutumia eneo la watu mashuhuri katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na kulazimika kuwapokea wageni wake wakiwemo hata majaji wakuu wa nchi zingine katika eneo la kawaida.