Hivyo ndivyo ulimwengu wa Sam Kolole ulivyompinduka siku moja wakati tamaa yake ya kujihusisha na mapenzi ya nje ya ndoa yalimpofanya kuambukizwa ugonjwa wa kisonono. Anasema kuteleza kwake kulimfanya kulia kama mtoto kwani kando na uchungu wa kupatwa na ugonjwa huo, ilikuwa kibarua kuanza kutafuta matibabu na alianza kujipata na fedheha kumueleza mkewe kwamba wangefaa kutibiwa wote pamoja kwa ajili ya utovu wa maadili yake.
Baada ya kupimwa na kupatikana na ugonjwa huo, Sam aliogopa kumuambia mkewe kuhusu kilichofanyika na hakujua iwapo alikuwa tayari ameshamuambukiza mkewe na ndiposa akajiamulia kwamba kabla ya kufahamu endapo mkewe pia ana ugonjwa huo, hatofanya mapenzi naye na hakushiriki naye tendo la ndoa kwa mwaka mmoja.
Hapo ndipo matatizo yake yalipoanzia kwani mkewe alianza kushangaa mbona Sam hakuwa akitaka kujamiana naye . Alitafuta vijisababu kila mara wakati mkewe alipotaka washiriki tendo la ndoa na hatimaye kwa sababu ya kuogopa kumueleza kilichokuwa kikifanyika, mkewe aliamua kumuacha na kuondoka .
Baada ya kutibiwa na kupona, Sam sasa amepata ujasiri wa kumueleza mkewe kilichofanyika na akitaka warudiane kumbe tayari mkewe alivyokwenda aligundua kwamba alikuwa pia na ugonjwa huo na akatibiwa alikokuwa amekwenda. Amekuwa na hamaki muda wote huo akikosa kuamini kwamba mumewe alikuwa akishiriki mapenzi hatari nje ya ndoa na hata kuambukizwa ugonjwa wa zinaa. Isitoshe, kando na tabia yake hiyo iliyohatarisha afya zao, aliogopa kumuambia naye pia apimwe ili kubaini ili kugundua iwapo ana ugonjwa huo .
Sam sasa ameachwa na majuto ya mbona hakumueleza mkewe wakati alipoambukizwa ugonjwa wa kisonono kwani hatua hiyo sasa imetishia kuigharimu ndoa yake. Wakati alipokwenda hospitalini kutibiwa, madaktari walisistiza kwamba aje na mwenzake ambaye walishiriki naye mapenzi. Sam hakuweza kuja naye kwa sababu anashuku alipata maradhi hayo kutoka kwa kahaba mmoja alipokuwa Kisumu safarini. Pia hangeweza kuja na mkewe kwa sababu angetakiwa kujibu maswali ambayo hakuwa tayari kutoa.