Mazuri yaja! Peter Kenneth akutana na wanasiasa kutoka Murangá

PK
PK
Wanasiasa kutoka Murang'a wamefanya mkutano na mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth katika hatua inayoonekana kama ya kumweka katika kapu la upande wa rais Uhuru Kenyatta baada ya mgombeaji huyo wa zamani kukutana na kiongozi wa ANC  Musalia Mudavadi anayedaiwa kutafuta ushirikiano na naibu wa rais William Ruto kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Seneta Irungu Kang'ata,  mbunge wa Maragua Mary Wamaua, Wangari Mwaniki wa Kigumo  na mbunge wa Gatanga  Nduati Ngugi  walikutana na PK katika hoteli ya   Greens huko Thika.

Wakati wa mkutano huo wa saa tatu waliahidi kushirikiana na Kenneth kuendeleza ajenda ya rais na kuliunganisha eneo la Mlima Kenya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kenneth amekuwa akipigiwa upato kwa uwezekano wa kujiunga na baraza la mawaziri na hata kutajwa kuwa miongoni mwa wanoweza kumrithi rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya.

Wiki jana, Kenneth alikuwa katika mkutano mwingine uliowaleta pamoja spika wa bunge  Justin Muturi,  waziri wa kilimo  Peter Munya,  magavana  Kiraitu Murungi (Meru), Ndiritu Muriithi (Laikipia),  na kiongozi wa wengi bungeni  Amos Kimunya  katika dhifa ya chakula cha mchana kwenye hoteli ya Panafric Hotel, Nairobi.

Magavana  Lee Kinyajui (Nakuru), Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi)  na seneta wa  Kirinyaga Charles Kibiru pia walikuwepo katika mkutano huo.

Kenneth anatayarishwa  kuwa mgombea mwenza au kwa nafasi ya ngazi ya juu  serikalini katika  muundo mpya wa utawala wa kisiasa utakaoundwa  endapo mapendekezo ya BBI yatapitishwa.