Mbadi apendekeza marekebisho ya kuwataka wanasiasa kueleza wanakotoa pesa za michango .

Maafisa wa serikali   ambao hutoa vitita vizito vya pesa katika hafla za  harambee hivi karibuni watatakiwa kuieleza tume ya EACC   walikozitoa pesa hizo . Marekebisho mapya katika  mswada wa watumishi wa umma (2019) yanayopendekezwa na kiongozi wa walio wachache bungeni John Mbadi  yanalenga kuwashurutisha wafanyikazi wa serikali wanaotoa  zaidi ya shilingi laki moja katika harambee  kuonyesha walikotoa pesa hizo  ndani ya kipindi cha siku 14 baada ya kutoa mchango wao .

Kwa mujibu wa  marekebisho hayo yanayopendekezwa na mbunge huyo wa suba kusini , unafaa kutangaza katika kipindi cha wiki mbili ulikotoa pesa hizo  baada ya kuzitoa wakati wa hafla ya kutoa mchango .

Amesema  pendekezo hilo jipya litasaidia kumaliza mtindo  wa sasa wa wanasiasa na watumishi wa umma kutoa  kiasi kikubwa cha pesa  katika hafla za michango ambapo baadaye hugunduliwa kwmba fedha hizo zimepatikana kupitia njia za ufisadi na uporaji wa pesa za umma .

Mbadi  anataka kurekebisha  sehemu za  13, 26, 28 na d 30  za sheria ya wafanyikazi wa umma ya mwaka wa 2003  ili kuhakikisha kwamba pesa  zilizopatikana kupitia njia za ufisadi hazitolewi katia harambee na kuwafumba macho wapiga kura .

Kumekuwa na majibizano  miongoni mwa wanasiasa kuhusu hatua ya baadhi yao kuonyesha kiasi kikubwa cha pesa ambazo huzitolewa katika michango na hasa kwa makanisa . Naibu wa rais  William Ruto amekuwa mstari wa mbele katika hafla kama hizo na marekebisho hayo ya Mbadi yanaonekana kumlenga . Ruto kwa upande wake ameshikilia kwamba anafahamu alikotoka katika ufukara na hivyo basi ataendelea kutoa msaada wa pesa kwa wakenya wanaohitaji usaidizi .

Suala hilo la michango na pesa zinazotolewa na wanasiasa limekuwa kubwa katika  mijadala ya kampeini za uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2022 .