Mbunge Milllie Odhiambo azungumzia kukosa mtoto

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo amefunguka na kusema yote kuhusu utasa wake na machungu ambayo amepitia maishani mwake kwa kukosa kupata mtoto.

Akizungumza siku ya Jumatano katika JKL Live, Millie hata hivyo alisema hali hii haijamfanya kuhisi kuwa mwanamke asiyekamilika.

“Mungu aliniumba kwa njia ya ajabu. Nahisi mkamilivu bila mtoto,” Millie alisema

Hata hivi, alisema anapanga kupata mtoto kupitia njia mbadala ya kufanikisha uja uzito kwa njia ya kiteknolojia mwezi Disemba.

“Nimejipa muda wa hadi Disemba ili kuamua kama nitafanyiwa oparesheni hiyo ya kufanikisha uja uzito kupitia teknolojia,” Millie alisema.

Mbunge huyo alisema kwamba aliguzwa sana na masaibu ya wanawake wasiokuwa na uwezo wa kupata watoto,hali iliyochangia yeye kuwasilisha mswada bungeni wa kufanikisha uja uzito kupitia teknolojia za kisasa .Millie aliongeza kwamba alikuwa na wakati mgumu kila alipopata hedhi.

“Nililazwa hospitalini kutoka na maumivu ya hedhi na kupungukiwa na damu. Kila wakati nilienda hospitalini niliambiwa nimeavya mimba," alisema.

“Wewe na hedhi zako ni kitu kimoja na zilitoka mbinguni kama kifurushi kimoja, furahia kuwa nazo.”

Aliongeza kwamba siku moja daktari alimwandikia kwamba alikuwa na maradhi ya zinaa, jambo ambalo alipinga akimweleza daktari kwamba alikuwa bado hajaanza kushiriki mapenzi.

Mbunge huyo alisema kwamba wanawake hupitia wakatu mgumu kila wanapotembelea madaktari kuhusiana na maswala ya uzazi na kudhaniwa kwamba wameavya mimba au wanaugua maradhi ya zinaa.

Millie aliwakashifu wale wanao wafanyia utani wasichana walio katika hedhi na kuwafanya kuhisi kukerwa na jambo hilo la kawaida. Mbunge huyo hivi majuzi alichapisha kwenye mtandao wa facebook kwamba ameamua kupata watoto wake akiwa na umri wa miaka 53.

Alisema kwamba amesalia jasiri kutokana na masaibu aliopitia ikiwemo dhana mbovu baadhi ya watu waliokuwa nayo dhidi yake.