Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri asalimisha bunduki kwa polisi

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amesalimisha bunduki yake kwa polisi.

Ngunjiri aliwasilisha bunduki yake katika afisi ya DCI mjini Nakuru siku ya Jumanne.

Aliwasili akiwa amebeba bunduki hiyo ndani ya kitabaa cheupe.

Ngunjiri ni mmoja wa maafisa wa serikali walioagizwa kusalimisha silaha zao kwa madai ya kuhusishwa na tuhuma za uhalifu. Magavana na wabunge wanaokabiliwa na kesi za ufisadi pia watapokonywa ulinzi wa serikali kufuatia agizo la Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai.

Agizo hilo jipya lamaanisha kwamba magavana wote, wabunge na viongozi wengine wanaopewa ulinzi na serikali na ambao wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu, ufisadi na mashtaka mengine watalazimika kutafuta ulinzi mbadala mbali na kusalimisha silaha zao.

Ngunjiri aliagizwa kufika mbele ya makao makuu ya DCI mjini Nakuru kuhusiana na matamshi yake wiki iliyopita kwamba naibu rais William Ruto alifurushwa kutoka makao yake rasmi mjini Mombasa.

Alifichua kwamba alikuwa ameagizwa kusalimisha bunduki yake na leseni ya kumiliki silaha hiyo. Punde tu baada ya kuwasilisha bunduki yake Ngunjiri alisema kwamba hilo halimtazuia kuzungumzia maovu katika serikali.

Alidai kwamba serikali imekuwa ikiwalenga viongozi wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto.

“Wanaweza kuchukuwa bunduki yao lakini hatutaogopa, tutaendelea kusema ukweli kuhusu nchi yetu,” alisema.