Mdosi ageuza mbochi kuwa mke, aaibishwa hadharani

download (1).jfif
download (1).jfif
Kioja kimeshuhudiwa  Nakuru mjini baada ya mama kumrushia cheche za maneno mdosi wa bintiye akimlaumu kwa kumfanya mkewe.

Duru ziliarifu kwamba binti alipata ajira katika duka moja la kutoa huduma za mpesa ambalo mamake alikuwa amemtafutia kazi.

Kwa mujibu wa taarifa, mrembo huyo anasemekana alikuwa mwenye bidii kama mchwa kwani aliichapa kazi kuanzia mapema asubuhi hadi jioni.

Hata hivyo, miezi michache baadaye inasemekana mdosi wake alianza kumnyemelea na mrembo naye akaingia 'box'.

Mrembo  alianza kwenda kwa jamaa kupika chakula cha mchana na hata jioni.

Kutokana na mazoea hayo, kidosho anasemekana aliacha kwenda nyumbani kwao kila jioni baada ya kazi na badala yake akaanza kulala kwa mdosi huyo ambaye walikuwa wamezama kwenye penzi.

Mama alianza uchunguzi wake pole pole na inasemekana alipigwa na butwaa kubaini kuwa bintiye alikuwa akilala kwa mwajiri wake.

Bila kupoteza muda, mama alinyanyuka moja kwa moja hadi kwa jamaa na kwa hasira akaanza kumkaripia vikali.

"Nani alikupa ruhusa ya kumfanya binti yangu mkeo? Tulikubaliana achape kazi asubuhi na jioni arejee nyumbani. Sijui ulitoa wapi ruhusa ya kumuita msichana wangu akupikie na kisha pia alale kwako," mama aliwaka.

Penyenye zinaarifu kwamba jamaa alibaki ameduwaa asijue la kusema huku msichana naye akihepa kupitia mlango wa nyuma kufuatia hasira za mama.

Kwa aibu jamaa alilazimika kumuomba mama msamaha mara nyingi zaidi huku mama akiapa kumchukulia hatua kali zaidia.

Haijajulikana iwapo mama alimshtaki jamaa jinsi alivyotishia au hata kama uhusiano wa jamaa na mrembo huyo uliendelea.