MERU: Kichwa cha mwanamke chakatwa kabla ya kutupwa shambani

Mchana wa Jumatano, wananchi wa kijiji cha Nkabune, Meru walishuhudia kifo kingine cha kinyama baada ya mwanamke kukatwa kichwa na kutupwa mita 30 mbali na mwili wake.

Mwanamke ambaye anajulikana kama Justa Mungania, mwenye umri wa miaka 25 na mama wa mtoto wa miaka miwili, alikuwa anaelekea kula chakula cha mchana nyumbani kwa nyanyake.

Mwanamke huyo alikuwa anafanya kazi za juakali na nyinginezo katika kituo cha Nkabune na alikuwa anaelekea kumyonyesha mwanawe.

Hata hivyo, hakufika na inakisiwa kuwa aligongwa kutoka nyuma na kifaa kikali.

Wanahabari na polisi walipofika katika eneo hilo, damu yake bado ilikuwa inaonekana katika eneo la tukio hilo na pia kutoka kichwani na mkononi mwake.

Wananchi ambao walifika hapo bado hawaelewi mbona mtu aliye na utu anaweza fanya jambo la kinyama kama hilo huku wengine wakikisia kuwa huenda ilikuwa ni kisa cha mzozo wa mapenzi, huku wengine wakihusisha mauji yale kama njia ya kutoa dhabihu.

Chifu wa eneo hilo, Kaari Muguna alisema kuwa aliambiwa kuhusu mauaji yake mda mchache baada ya saa saba siku ya Jumatano.

“Nilipokea simu kuwa mwanamke aliuawa na nilipofika katika eneo hilo nikapata mwili bila kichwa. Tulipofuata matone ya damu tukapata kichwa kati shamba lililoko hapo karibu." Muguna alisema.

Muguna aliwahakikishia wakaazi kuwa ataboresha usalama.

Chifu huyo alisema kuwa kijana wa shule alisema kuwa alimuona mtu akiingia shambani ambapo kichwa cha mwanamke huyo kilipatikana.

-Dennis Dibondo