Katika kinachonekana kama kudorora zaidi kwa uhusiano kati ya viongozi hao wawili , washirika wa Ruto wanaoshikilia nafasi za uongozi chamani, wanasema chama hicho kilitoa zaidi ya shilingi milioni 183 mwaka wa 2018 ambazo matumizi yake hayajaelezwa ifaavyo.
Naibu katibu mkuu wa chama Caleb Kisitany ambaye ni mshirika wa Ruto ametaka kupewa stakabadhi za keleza jinsi mamilioni hayo yalivyotumiwa lakini katibu mkuu Raphael Tuju amempepezea chini akisema matakwa yake hayo ni sarakasi tu za kisiasa kwa sababu hana uwezo au mamlaka ya kutaka kuchunguza madai hayo.
Kositany anataka kupewa stakabadhi mbalimbali zikiwemo taarifa za benki za akaunti za pesa za Chama cha Jubilee kwa muda wa miaka 4 iliyopita. Yadaiwa Kositany ni miongoni mwa washirika wa Ruto watakaopigwa shoka kutoka nafasi za uongozi katika chama cha Jubilee.
Kositany ameshangaa mbona chama hicho kinalipa kodi ya jengo zima la makao makuu ya Jubilee ilhali hakitumii jengo zima na pia kuhoji kutolewa kwa mamilioni ya pesa kulipa kodi za matawi ya chama ilhali hayajakuwa yakiendelea na oparesheni zozote.
Wawakilishi wa kaunti wa Chama cha Jubile wamekuwa wakitoa shilingi 5000 kila mwezi, wabunge elfu 20 na magavana shilingi elfu 50 kila mwezi kwa chama hicho kwa miaka saba iliyopita.
Chama hicho kina wabunge 171 katika mabunge yote mawili hatua inayomaanisha kwamba wamekuwa wakikusanya shilingi milioni 3.4 kila mwezi. Magavana wote 25 wa Jubilee hutoa pato la shilingi millioni1.2 kila mwezi kando na mamia ya wawakilishi wa kaunti ambao pia hutoa michango yao chamani.
Wabunge wake watano wa EALA hutoa shilingi 20,000 kila mwezi. Hatua ya kutaka stakabadhi za kifedha za chama imejiri baada ya washirika wa Ruto chamani humo kupa kusalia ndani ili kuendeleza mapambano yao wakiwa ndani ya Jubilee.