Mhubiri akamatwa akifukua miili ya wafu Naivasha

coffin pic
coffin pic
Polisi mjini Naivasha wamemkamata mhubiri mmoja aliyepatikana akifukua miili ya jamaa 7 waliofariki miaka kadha iliyopita.

Askofu huyo wa dini ya Akorino huko Kinamba alikua tayari ameifukua miili mitatu ukiwemo wa mkewe, kabla ya polisi na maafisa wa afya ya umma kumfumania.

Mhubiri huyo ambaye hata hakuonekana kushtuka alikiri kuifukua miili hio akisema alitaka kuizika mahala kwingine ili auze kipande hicho cha ardhi kwa wachimba migodi.

Askofu huyo Samuel Macharia alijitetea akisema alijaribu kutafuta agizo la mahakama lakini mchakato huo ulikua unachukua muda mrefu.

Alisema aliamua kuifukua mwenyewe miili hio kwani ilikua ghali mno kuajiri wataalamu wa kazi hio.

“Nina kipande kingine cha ardhi ambacho nilitaka kuizika tena miili hio lakini nadhani ingekua bora iwapo ningesubiri agizo la mahakama,” alisema.

Miongoni mwa miili ambayo mhibiri huyo alikua tayari ameifukua ni pamoja na wa mkewe, mwanae na mamake kabla ya polisi kumkamata.

Kufuatia kisa hicho majirani na jamaa zake walimtete mhubiri huo wakisema ni kawaida kwa watu wa eneo hilo kuhamisha makaburi ili kukodisha ardhi yao kwa wachimba migodi.

Mpwawe Rebecca Wambui alisema kua oparesheni hio ilitekelezwa usiku na kua alishtuka kupata makaburi hayo yamefukuliwa, asubuhi.

“Alikua ametuambia kua atayahamisha makaburi hayo lakini shida ni tu alikosa kuhusisha taasisi za serikali ,” alisema Wambui.

Akiongea kwa njia ya simu OCPD wa Naivasha Samuel Waweru alithibitisha kisa hicho akisema miili iliyofukuliwa imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Naivasha, huku mshukiwa akizuiliwa kusubiri kufikishwa mahakamani.