Mhubiri ashtakiwa kwa kutumia jina la Uhuru kulaghai familia ya Akasha

AKASHA
AKASHA
Walaghai akiwemo mhubiri walitumia jina la rais Uhuru Kenyatta kuilaghai familia ya Ibrahim Akasha shilingi milioni 5.5 wakiahidi kuwarejesha nchini jamaa zao kutoka jela za Marekani.

Baktash Akasha alihukumiwa miaka 25 gerezani mnamo Agosti 16 huku Ibrahim Akasha akisubiri kuhukumiwa Novemba 8 kuhusiana na ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Marekani.

Kutokana na tamaa na masumbuko ya kutaka jamaa zao warejee nyumbani, Najma Hassan alijipata katika mtego wa walaghai waliojidai kuwa na uhusiano wa karibu na wakuu katika serikali.

Alimlipa Mhubiri Chris Ngweti pesa baada ya kudai kutumwa na rais Uhuru Kenyatta. Ngweti alishikwa na kushtakiwa siku ya Alhamisi. Stakabadhi za mashtaka dhidi yake zasema kwamba kati ya Oktoba 9 na Novemba 15, mwaka 2018, Ngweti alikutana na Najma Hassan, mke wa Baktash, akishirikiana na watu wengine, alijipatia pesa kutoka kwa Najna kwa njia ya ulaghai.

Mshukiwa alikanusha mashtaka alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mkaazi David Odhiambo.

Aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu au bondi ya shilingi milioni mbili na mdhamini wa kiasi sawa na hicho. Najma alikuwa amepoteza matumaini na alikuwa nyumbani baada ya kushindwa kumrejesha nyumbani mumuwe alipopokea simu kutoka kwa afisi ya DCI eneo la Kisauni.

“Tulikuwa twazungumza ndiposa nikamweleza masaibu yalionikumba. Akanishauri kuandikisha taarifa na uchunguzi ukaanza,” Najma alisema.

Katika taarifa yake, Najma alisema kwamba alimueleza Ngweti, ambaye ni pasta wake katika kanisa eneo la Shanzu ambapo wakati mwingine yeye huenda kwa maomba, akitafuta usaidizi kuwarejesha nchini kaka hao wa Akasha. Pasta huyo alikubali kumuunganisha na mtu mashuhuri ambaye angemsaidia kukutana na rais Uhuru Kenyatta ili apate usaidizi.

Ngweti kisha alimtambulisha Najma kwa Steven Nzioka ( Steve) mkaazi wa Nairobi aliyezungumza kana kwamba ni mtu tajika katika safu za serikali. Steve alimtaka wakutane Nairobi siku iliyofuata ili kufanikisha mpango wake. Najma ,alifunga safari ya Nairobi kutoka Mombasa akiandamana na bintiye, Hayat Akasha, wifi wake na mama mkwe.

Walikutana na Steve mtaani South B ambapo walikuwa wanaishi na akawahakikishia kuwa mambo yalikuwa shwari. Steve anasemekana kuambia kwamba kwa vile ilikuwa wikendi, rais alikuwa na familia yake na kwamba wangekutana naye siku ya Jumatatu.

Hata hivyo aliwaitisha shilingi laki tano, kwa madai kwamba pesa hizo atampa msimamizi wa Ikulu Kunuthia Mbugwa ili afanikishe mkutano na rais. Siku ya Jumatatu Steve aliwachukuwa jamaa hao wa Akasha mwendo wa saa mbili za asubuhi na kuwapeleka katika Hoteli ya Grand Regency waliko kaa hadi saa kumi na mbili jioni.

Mwendo wa saa kumi na mbili jioni, aliwambia kwamba ameagizwa kukutana na waziri wa Mambo ya kigeni Monica Juma ambaye angewapa barua ya kuwarejesha nchini kaka wa Akasha. Aliitisha tena shilingi laki tano ambazo alipewa na Hayat. Aliondoka na pesa hizo mwendo wa saa moja jioni akidai kwamba atalazimika kusubiri hadi barua hiyo iandikwe ili awape.

“Tulisubiri hadi saa tatu usiku na kisha kuondoka kwa teksi alipokosa kurudi,” Najma alisema.

Asubuhi iliofuata Najma alimpigia simu Steve mara tatu lakini hakujibu simu. Baadaye Steve alimpigia na kumjulisha kwamba alikuwa anafuata taratibu ambazo zilikuwa zachukuwa muda. Aliwahakikishia tena kwa mambo yalikuwa shwari. Baada ya siku tatu, Oktoba 12, 2018, Steve aliwasili mtaani South B alipokuwa anaishi Najma mwendo wa saa tatu usiku na barua. Barua aliodai ilikuwa imeandikwa na waziri Monica Juma kwa ubalozi wa Amerika, ilikuwa haina tarehe na haikuwa na sahihi.

“Kisha aliondoka akidai kwamba alikuwa anaipeleka kutiwa mhuri na saini. Alisema kwamba alikuwa tu ameleta kutuonyesha ili tujuwe kwamba shughuli ilikuwa yaendelea,” Hayat alinakili.

Baada ya siku chache alirejea na barua nyingine kutoka afisi ya rais ilioandikwa tarehe 19 Oktoba mwaka 2018, ikidaiwa kutiwa saini na msimamzi wa Ikulu Kinuthia Mbugwa na nakala moja kupewa waziri wa mambo ya kigeni. Alipotea tena na kurudi baada ya siku nne akiitisha “kitu” cha rais” kwa sababu waziri tayari alikuwa amewasiliana naye.

Pesa hizo kulingana na Steve zilikuwa zifanikishe kuandikwa kwa barua na rais, ya kutaka kaka wa Akasha kurejeshwa nchini.

“Mamangu alimpa shilingi milioni moja na akatoka nje kupiga simu. Aliporudi, alisema kwamba rais amekataa na alitaka shilingi milioni tatu,” Hayat aliripoti.

Steve aliondoka majira ya adhuhuri na kusema kwamba angerudi kuchukuwa pesa zilizosalia. Mwendo wa saa kumi alasiri alirejea na kupewa shilingi milioni 1.5. Baadaye usiku huo, Steve alirudi na barua nyingine aliodai ni ya kutoka idara ya kukabiliana na mihadarati ya Amerika yenye nambari ya kumbukumbu 15/11/201 kutoka jamaa kwa jina Abdalla. Alidai kwamba “Rais’ alikuwa amemuagiza Abdalla kushughulikia swala hilo.

Familia hiyo kisha ilirejea Mombasa, Steve aliwafuata Mombasa akidai kwamba alitaka kuwasaidia kuondoa kesi ya Akasha kutoka mahakamani. Kwa shughuli hii alititisha shilingi milioni 1.5. Wakati huu aliandamana na Pasta Chris na kukutana na Najma na bintiye katika hoteli karibu na Fort Jesus.

“Kwa majuma mawili alinizungusha na kushindwa kutimiza ahadi yake ya mwisho” Najma aliambia polisi.

Steve kisha aliambia Najma kwamba Rais alikuwa amerejea nchini na kwamba wangeenda kumpokea katika uwanja wa ndege mjini Nairobi. Familia hiyo ilifunga safari, wakati huu wakiandamana na jamaa wengi wa familia hiyo.

“Alitupeleka katika hoteli kukaa kwa siku nne huko. Alituambia tusiwe na hofu na kudai kwamba rais na mamake walikuwa pia wanaishi katika hiyo hoteli,” Najma aliripoti.

Steve aliwaambia kwamba walinzi wa marekani wangewachukuwa na kuwapeleka kukutana na rais.

Baada ya kuzungushwa na Steve, Najma alimwambia wanarejea Mombasa, Najma alisema hiyo ndio ilikuwa mara ya mwisho walisikia mambo ya Steve. Kesi hiyo itatajwa Novemba 14 katika Mahakama ya Shanzu.