Mhubiri Uganda akamatwa kwa kusema hakuna coronavirus Afrika

Polisi jijini Kampala, Uganda wamemkamata kasisi mmoja kwa kutamka matamshi yasiyo ya kweli na kueneza propaganda kuhusu ugonjwa wa Coronavirus.

Mhubiri huyo anadaiwa kutumia stesheni yake ya runinga kuwaambia umma kuwa ugonjwa huo haupo barani humu huku akidai kuwa hakuna kifo hata kimoja kimeripotiwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Hayo yakijiri, idadi ya watu ambao wamegunduliwa kuwa na virusi vya Corona nchini Uganda imeongezeka kutoka wagonjwa kumi na 18 hadi 25 baada ya watano kupimwa siku ya Ijumaa.

Serikali sasa imewataka waganda kuzingatia kwa kina mikakati iliyowekwa ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Tukirejea nchini, serikali inahimizwa kubadili marufuku ya kutotoka nje ili iwe ya kuanzia saa tatu usiku ili kuwaruhusu wanaotekeleza huduma muhimu kufika nyumbani kutoka wanapoondoka kazini.

Mwenyekiti wa muungano wa wamiliki matatu Simon Kimutai anasema washikadau katika sekta ya usafiri wa umma wako tayari kuafikiana makubaliano ili tatizo la kuongezwa ka nauli lisuluhishwe.