Miaka 50 tangu kifo cha Tom Mboya, Je kwanini aliuawa?

Mboya (1)
Mboya (1)
Ni miaka 50 sasa tangu aliyekuwa waziri katika serikali hayati mzee Jomo Kenyatta, Thomas Joseph Odhiambo Mboya alipouawa kwa kupigwa risasi katikati mwa jiji la Nairobi.

Tom Mboya kama alivyojulikana na wengi alipigwa risasi Julai tarehe 5, mwaka 1969 alipokuwa anaondoka baada ya kununua dawa katika duka la kuuza dawa la Chhanni’s kwenye barabara ya Moi Avenue, iliyokuwa ikijulikana kama Government Road.

Mshukiwa wa mauaji yake Nahashon Njoroge alikamatwa na polisi muda mfupi baada ya mauaji hayo, lakini mwezi Septemba mwaka huo idara ya polisi ilitangaza kwamba alikuwa ameaga dunia katika hali ya kutatanisha.

Hadi sasa bado haijabainika kiini na nina aliagiza kuuawa kwa Mboya.

Kulingana na ripoti ya polisi Tom Mboya aliuauwa Jumamosi asubuhi akiwa dukani wakati mwanamume mmoja ambaye kulingana na uchunguzi wa awali ni kama alikuwa amemfuata kabla ya kumfyatulia risasi alipokuwa akiondoka dukani baada ya kununua dawa.

Kutangazwa kwa kifo chake kulipelekea maandamano katika miji mikuu nchini huku hisia kali zikisheheni mazishi yake eneo la Rusinga Island. Mboya anakumbukwa kwa weledi wake wa kupanga maneneo katika hotuba zake na ustadi katika lugha ya Kingereza.

Alizaliwa mwaka wa 1930 na kufariki mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 39. Alichangia sana katika mikakati ya kutetea maslahi ya wafanyikazi nchini na kusaidia kuanzisha vyama vya kutetea maslahi ya wafanyikazi. Chuo cha mafunzo ya Leba cha Tom Mboya mjini Kisumu kimeitwa jina lake kutambua mchango wake katika kutetea wafanyikazi.