Michael 'Engineer' Olunga asaidia Kenya kuigaragaza Tanzania

Mabao mawili ya Michael Olunga yaliisaidia Harambee kutoka nyuma na kuwacharaza majirani Tanzania 3-2, katika kipute kinachoendelea cha AFCON nchini Misri, na kusalia kwenye kinyang’anyiro cha 16 bora, kwa mara ya kwanza.

Tanzania walianza kufunga mabao mawili kupitia kwa Simon Msuva na Mbwana Samatta lakini dakika moja baadae Olunga akasawazisha na kisha kufunga bao la pili kunako dakika ya 80 baada ya Johana Omolo kufunga bao pia, na kuisadia Kenya kupanda hadi katika nafasi ya tatu katika kundi C wakiwa na alama tatu sawia na Senegal.

Awali Algeria walijikatia tikiti ya 16 bora na ushindi wa 1-0 dhidi ya Senegal, kupitia kwa bao la Youcef Belaili.

Tanzania wako chini kwenye orodha hio wakiwa bila ya alama lakini huenda wakafuzu iwapo watawanyuka Senegal katika mechi ya mwisho.

Madagascar nao waliwacharaza Burundi 1-0 na kupanda hadi wa pili katika kundi B wakiwa na alama 4 nyuma ya Nigeria ambao wamefuzu tayari.

Katika msururu wa spoti bara Uropa, Patrick Vieira ni miongoni mwa majina ambayo Newcastle United inatathmini kuchukua nafasi ya Rafael Benitez kama meneja.

Benitez ataondoka St James' Park baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu ambapo mkataba wake unatamatika tarehe 30 mwezi huu. Mfaransa huyo amemaliza kampeni yake ya kwanza kama meneja wa Nice, na hana haraka ya kuhama lakini atasikiza ofa watakayotoa.

Tukisalia Uingereza, Aaron Wan-Bissaka amemaliza uchunguzi wake wa kimatibabu Manchester United na tangazo maalum kuhusiana na uhamisho wake Old Trafford linatarajiwa kufanya hii leo.

Mlinzi huyo wa miaka 21 alimaliza awamu ya pili ya uchunguzi wake huko Carrington jana kabla ya kuondoka Crystal Palace. Muingereza huyo anakua mchezaji wa pili kusajiliwa na United, baada ya winga wa Wells Daniel James kusajiliwa kutoka Swansea.