Watford yashangaza Arsenal baada ya kutoka nyuma na kutoka sare

watford
watford
Watford walijitahidi kutoka nyuma mabao mawili kufikia muda wa mapumziko na kutoka sare na Arsenal kwenye mechi ya kwanza ya Quique Sanchez Flores tangu kuteuliwa kama meneja wa Hornets.

Walisawazisha wakati Roberto Pereyra kufunga penalti ya dakika za mwisho baada ya Tom Cleverley kupunguza pengo hilo na kupata alama yao ya pili tu msimu huu. Pierre-Emerick Aubameyang alikua amewaweka wageni mbele kwa mabao mawili baada ya kufunga kutoka kwa pasi ya Sead Kolasinac na Maitland-Niles.

Hayo yakiji, kiungo wa Arsenal Henrikh Mkhitaryan ambaye yuko Roma kwa mkopo alifunga bao lake la kwanza AS Roma walipowanyuka Sassuolo 4-2 katika mechi ya Serie A.

Raia huyo wa Armenia alifunga bao la tatu la timu yake baada ya Bryan Cristante kufunga bao la kichwa na lingine kutoka kwa Edin Dzeko kuwaweka Roma mbele.

Justin Kluivert alifanya mambo kuwa 4-0 lakini Domenico Berardi akafungia Sassuolo mabao mawili. Ushindi huu ulikua wa kwanza wa Roma msimu huu.

Kwingineko, meneja Rudi Gutendorf, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya Guinness kwa kufunza timu 55 katika mataifa 32 kwenye mabara matano, amefariki akiwa na umri wa miaka 93.

Tajriba ya Gutendorf ya ukufunzi ilidumu kwa nusu ya karne, ikiwemo timu za ngazi za juu katika nchi yake Ujerumani, na timu za 18 za kimataifa ikiwemo Australia, Uchina na Fiji. Gutendorf pia alikua meneja wa mataifa 7 barani Afrika zikiwemo Botswana, Tanzania, Sao Tome e Principe, Ghana, Mauritius, Zimbabwe na Rwanda.

Tukirejea humu nchini, ndoto ya Gor Mahia ya kufuzu kwa raundi ya makundi ya ligi ya mabingwa ya Caf ilipata pigo kubwa baada ya kulazwa mabao 4-1 na USM Alger kwenye mkondo wa kwanza.

Makosa ya ulinzi yaliwapa wenyeji fursa ya kufika katika eneo la hatari huku raia wa Morocco Muaid Ellafi akifanikiwa kufunga bao. Mohamed Meftah pia hakusita na kufunga bao. K'ogalo sasa wanahitaji angalau mabao 3-0 katika mkondo wa pili nyumbani ili kuwabandua Algeria.

Malkia Strikers walipoteza kwa Uholanzi katika mechi yao ya pili kwenye michuano ya kombe la dunia ya FIVB huko Japan. Kama tu katika mechi yao ya ufunguzi jumamosi dhidi ya Marekani, Malkia walianza kwa kujikokota kwenye seti ya kwanza na kujitahidi katika mbilizi zilizofuata kwa kuonyesha mchezo mzuri.

Mercy Moim aliongoza kwa alama 9, Violet Makuto alikua na alama 7 huku Sharon Chepchumba akipata alama 6.

Geoffrey Kamworor aliipiku rekodi ya dunia kwa dakika 17 katika mbio za Copenhagen Half Marathon jana, aliposhinda mbio hizo za IAAF Gold Label kwa dakika 58 na sekunde 1. Ushindi huo wa mwanariadha huyo wa miaka 26 ulitokea katika nchi ambayo alishinda mataji yake matatu ya kwanza katika mbio za marathon za dunia mwaka 2014.