Serikali kulipa marupurupu ya Kenya 7s, kinadada wawachwa nyuma?

Serikali imejitolea kuwalipa timu ya raga nchini marupurupu yao ya michuano ya kufuzu kwa Olimpiki iliyochezwa wikendi iliyopita. Wizara ya michezo imeomba taarifa za benki za wachezaji wote ili kuweza kuwalipa, baada ya timu hiyo kuinyuka Uganda 31-0 na kufuzu kwa michuano hiyo.

Hata hivyo hakukua na taarifa zozote kuhusu marupurupu ya timu ya kinadada ambao pia walifuzu kwa Olimpiki. Hii ni licha ya kinadada hao kumrai waziri Amina Mohammed kuingilia kati.

Hayo yakijiri, Tottenham wanatarajia kumchukua mshambuliaji wa kati wa timu ya Roma ya Italia Lorenzo Pellegrini, mwenye umri wa miaka 23, kama mtu anayeweza kuchukua nafasi ya Christian Eriksen. Kwingineko Nemanja Matic anataka kuondoka Manchester United, ikiwezekana mwezi Januari, huku kiungo huyo wa kati Mserbia mwenye umri wa miaka 31 akitarajiwa kwenda Italia.

Miamba wa soka Uhispania Real Madrid wanatathmini kitita cha Uro milioni 400 kumsajili nyota mshambulizi wa PSG Kylian Mbappe. Raia huyo wa Ufaransa alihusishwa na uhamisho hadi Los Blancos wakati alipokua akichezea timu ya Ligue 1 AS Monaco lakini akahamia PSG kwa kitita cha Uro milioni 135.

Mbappe mwenye umri wa miaka 20 awali alihusishwa na uhamisho wa mabingwa hao wa Uropa lakini kwa mujibu wa ripoti za hivi punde Madrid wanamtaka sana mshambulizi huyo na wako tayari kutoa kitita hicho.

Manchester United hawana uhakika atakaporegea Scott McTominay baada ya kupata jeraha la mguu. Kiungo huyo wa kati alijiondoa kutoka kwa kikosi cha Scotland baada ya kufanyiwa uchunguzi jumatatu akiwa na tatizo hilo tangu alhamisi iliyopita waliposhinda mechi yao ya ligi ya Uropa dhidi ya Partizan Belgrade.

McTominay, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa wacheza anaowategemea Ole Gunnar Solskjaer msimu huu, alianza katika ushindi wao dhidi Brighton wikendi lakini akalazimika kuondoka mwishoni mwa mechi hio kwani alionekana kuwa na uchungu mno.