Ancelotti apigwa kalamu na Napoli, Chelsea na Liverpool wafuzu Champions League

ancelotti
ancelotti
Carlo Ancelotti amepigwa kalamu kama Kocha wa Napoli baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miezi 19. Vyombo vya habari vya Kiitaliano vilitangaza mapema jana kuwa Mkufunzi wa zamani wa AC Milan Gennaro Gattuso ndiye anatarajiwa kuongiza klabu hiyo.

Napoli ilitangaza kutimuliwa kwake saa chache baada ya kupigwa mabao  4-0 na Genk. Mwezi uliopita Mkufunzi huyo na wachezaji wa Napoli walikuwa kwenye malumbano na rais Aurelio de Laurentiis baada ya kutoa agizo kwa timu hiyo kufanya mazoezi kwa wiki moja jambo alilokataa Ancelotti na Wachezaji wake.

Liverpool iliikwaruza Red Bull Salzburg kwa kujizolea mabao 2-0. Mabao hayo yaliyotingwa na Nabby Keita na Mohammed Salah yaliiondoa Red Bull kwenye jedwali.

Kwingineko Chelsea ilinusurika kupata kovu lisilosahaulika ligini kwa ushindi 2-1 dhidi ya Lille uwanjani Stamford Bridge.

Jose Mourinho anasisitiza kuwa  kujifunza kwake Kijerumani hakuna uhusiano wowote na kazi huku akiongeza kuwa hana mipango yoyote ya kuiacha Tottenham na kuhamia Bayern Munich.

Hapo awali inadaiwa kuwa Bayern walitaka kumwajiri Mourinho baada ya kumpiga kalamu Niko Kovac mwanzo wa mwezi Novemba. hata hiyo Mourinho baada ya wiki mbili alipata kazi yake mpya na kuchukua nafasi ya Mauricio Pochettino katika klabu ya Tottenham na kuiacha Bayern ikimtafuta kocha atakayechukua nafasi ya Kovac.

Bologna wamewasiliana na klabu mbili za ligi ya Premia kuhusu mshambulizi wa Wolves Patrick Cutrone, mwenye umri wa miaka  21, na mshambulizi wa Everton mwenye umri wa miaka 19 Moise Kean. Mkurugenzi wa Bologna Walter Sabatini amesema hakuna uwezekano wowote wa kumsajili Zlatan Ibrahimovic baada ya kufichua kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka thelathini na minane  tayari ameamua  atakakohamia.

Sofapaka imeandikisha ushindi wake wa sita kwenye ligi kuu nchini KPL baada ya kuichapa Kisumu All Stars mabao 2-1 hapo jana kwenye uga wa  Kenyatta uliojaa matope mjini Machakos.

Ushindi wa mabingwa hao wa mwaka 2009 uliipelekea Kisumu kupoteza mechi yake ya 8. Aidha Nahodha wa All Stars Gerishom Arabe amelalamikia hali mbovu ya uwanja huo.