Mshambulizi wa Tanzania Samatta, awindwa na vilabu vya Uingereza

samatta
samatta

Klabu za Norwich na Brighton zimeulizia kuhusu mshambuliaji wa Genk na Tanzania Mbwana Samatta.

Akiwa na thamani ya £10m, amefunga magoli 10 msimu huu matatu katika ligi ya mabingwa dhidi ya Liverpool na RB Salzburg.

Pia mchezaji huyo amevutia klabu kama vile Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na Lazio ya Itali.

Samatta mwenye umri wa miaka 27 alikuwa mfungaji bora katika ligi ya Ubelgiji msimu uliopita akifunga magoli 25 na kuisaidia Genk kushinda taji lao la nne la ligi katika historia yao.

Samatta pia alitawazwa kuwa mshindi wa taji la Ebony Shoe mwaka uliopita ambalo hutolewa kwa mchezahi bora wa Afrika nchini Ubelgiji.

Mchezaji huyo wa kimataifa awali alihusishwa na uhamisho wa klabu kadhaa za Uingereza ikiwemo Leicester, Aston Vill na Watford.

Msimu uliopita kulikuwa na tetesi kwamba nyota hyo alikuwa akinyatiwa na klabu kama vile West Ham, Everton na Burnley.

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.

Amesalia na miezi kadhaa hivi kabla ya mkataba wake kumalizika.

Samatta alihamia Ubelgiji mwaka mmoja baada yake kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Mwafrika aliyekuwa anacheza ligi za barani Afrika mwaka 2015.

Alishinda vikombe sita vikuu akiwa na TP Mazembe ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kuondoka.

Kufikia Machi mwaka huu, alikuwa ameichezea timu ya taifa ya Tanzania mechi 44 na kuwafungia mabao 16 tangu alipowachezea mara ya kwanza mwaka 2011.

Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.

Ingawa Mtanzania huyo amevuma sana msimu huu, ambapo alifunga mabao manane katika mechi 11 za kwanza, msimu uliopita hakufanya vyema sana. Alifunga mabao saba katika mashindano yote akichezea klabu yake msimu wa 2017/18.

-BBC