Chelsea wafanya mazungumzo ya kumsajili wing'a Ziyech kutoka Ajax

ziyech
ziyech
Chelsea wanafanya mazungumzo ya kumsajili wing’a wa Ajax Hakim Ziyech msimu huu wa joto kwa kitita cha pauni milioni 38, kwa mkataba ambao huenda ukatangazwa hivi karibuni.

Meneja wa Chelsea Frank Lampard alitaka kumsajili mchezaji huyo wa miaka 26 mwezi Januri, lakini klabu yake haikutaka kumuuza wakati huo. Mchezaji huyo raia wa Morocco atakuwa wa kwanza kusajiliwa na Chelsea kufuatia kuondolewa kwa marufuku yake ya kusajili wachezaji.

Chelsea walitaka kuwasajaili wachezaji kadha mwezi  Januari ikiwemo kiungo wa Paris St-Germain Edinson Cavani na mshambulizi wa Napoli Dries Mertens.

Mshambulizi wa Real Sociedad Willian Jose yuko katika orodha ya Barcelona ya wachezaji inaotaka kuwasajili, baada ya kupewa ruhusa na mamlaka nchini Uhispania ya kumsajili atakayechukua nafasi ya Ousmane Dembele. Kiungo huyo raia wa Brazil alikuwa amehusishwa na kuhamia Tottenham na Manchester United mwezi uliopita, na alikosa mechi tatu za Sociedad Januari, baada ya kutaka kukaa kando hadi hatma yake ijulikane.

Dembele, ambaye hajachezea Barcelona tangu Novemba hatacheza kwa muda wa msimu uliosalia kutokana na jeraha la paja.

Manchester United iko tayari kuipiku Chelsea katika kinyang'anyiro cha kutoa dau la pauni milioni 120 kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund na Uingereza Jadon Sancho mwenye umri wa miaka 19.

Kwingineko Liverpool inajiandaa kumpatia beki wa Uholanzi Virgil van Dijk wa miaka 28, mkataba mpya wenye thamani ya zaidi ya pauni elfu 150 kwa wiki.

Kocha wa Gor Mahia Steve Polack na wa KCB Zedekiah Otieno wamewasuta marefa wa KPL kwa kile wanachotaja kuwa usimamizi usio wa haki wakati wa mechi zao hapo jana.

Mabingwa Gor Mahia walitoka sare ya 1-1 na Western Stima huku KCB wakipoteza 2-1 kwa Bandari. K’Ogalo walisalia na wachezaji 10 baada ya mlinzi Joash Onyango, kupewa kadi nyekundu, ambayo Polack anasema haikuwa sawa. Stima pia waliishia na wachezaji 10 baada ya Villa Oromochan kuondolewa uwanjani kunako dakika ya 75.

Huko pwani Zico naye alilalamikia usimamizi mbovu wa mechi uliompelekea kupoteza kwa wenyeji.

Kushiriki kwa Mohamed Salah katika michuano ya Tokyo mwaka 2020 kutategemea uamuzi wake na klabu yake ya Liverpool, kulingana na kocha wa Misri Shawky Gharib.

Salah yuko katika orodha ya Misri ya wachezaji 50 kwa kipute hicho ambacho fainali yake itakuwa Agosti tarehe 8, ambayo pia ni siku ya kwanza ya mechi za msimu wa ligi ya Primia wa mwaka 2020-21.

Kipute hicho ni cha wachezaji wa umri wa chini ya miaka 23, lakini wachezaji watatu wa umri uliopita wanaruhusiwa.